1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaomba ahadi mpya kwa ajili ya UNRWA

26 Juni 2018

Umoja wa Mataifa umewaomba wanachama kujaza pengo la kifedha baada ya rais Donald Trump wa Marekani kukata ufadhili uliosaidia katika uendeshwaji wa programu za kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina.

https://p.dw.com/p/30IH9
Flüchtlinge aus Afghanistan in Griechenland
Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa umeyaomba mataifa wanachama kujaza pengo kubwa la kifedha lililosababishwa na hatua ya serikali ya rais Donald Trump wa Marekani, kukata ufadhili uliosaidia katika uendeshwaji wa programu za kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina katika eneo lote la Mashariki ya Kati. 

Umoja wa Mataifa ulifanya mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya huduma muhimu kuanzia misaada ya chakula na vifaa tiba hadi usafi, kwa ajili ya wakimbizi milioni 5 walioko ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, Jordan, Lebanon na Syria.

Baada ya vikao kumalizika, bado ulikuwa ukipiga mahesabu ya kiwango cha fedha kilichoahidiwa na kila mwanachama, dhidi ya kiwango kilichopungua kwa mwaka huu cha dola milioni 250, kinacholikabili shirika la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina, na linalosimamia juhudi za utoaji wa misaada ya kiutu, UNRWA.

Pierre Krähenbühl
Mkuu wa UNRWA, Pierre Krahenbuhl amesema kuna upungufu mkubwa wa kifedha, unaotishia utoaji wa huduma muhimu za kibinaadamu kwa wakimbizi wa Palestina.Picha: DW/M. Estarque

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema Marekani, ambayo ni mchangiaji mkubwa zaidi, ilitoa dola milioni 364 kwa shirika hilo mwaka jana, lakini limetoa dola milioni 60 tu kwa mwaka huu. Mkurugenzi wa UNRWA, Pierre Krahenbuhl amesema punguzo hilo la ufadhili linaathiri utoaji wa huduma muhimu kama chakula katika eneo la Gaza, pamoja na huduma za tiba katika vituo vya afya, wakati takriban watoto 500,000 huenda wakashindwa kuanza shule mwaka huu.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema hii leo kwenye mkutano wa kupokea ahadi za michango unaofanyika mjini New York Marekani kwamba kushindwa kuiwezesha UNRWA kupata rasilimali kutakuwa na madhara, ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa ugumu kwa jamii inayohitaji misaada, kukosekana kwa matumaini ya kikanda na hata  utulivu kwa duniani.

Karibu watu milioni 2 katika eneo la ukanda wa Gaza, wanawake na watoto tayari wamekwishakumbana na athari za upungufu mkubwa wa maji na umeme, katika wakati ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya Waisrael na Wapalestina, hasa baada ya Marekani kufungua ubalozi wake mjini Jerusalem. 

Serikali ya Trump ilitangaza mnamo mwezi Januari kuondoa ufadhili wa dola milioni 65, iliyokuwa sehemu ya mpango wa ufadhili wa serikali yake ya dola milioni 125 kwa ajili ya misaada ya kiutu kwa wakimbizi hao. Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba haoni sababu ya kutoa fedha nyingi za Wamarekani, wakati hawapati shukrani wala heshima kutoka kwa Wapalestina.

Mwandishi: Lilian Mtono/ape/dpae.

Mhariri: Iddi Ssessanga