1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yamuwekea vikwazo Laurent Gbagbo

31 Machi 2011

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha bila pingamizi zozote vikwazo dhidi ya Laurent Gbagbo anayeng’ang’ania madaraka nchini Cote d’Ivoire.

https://p.dw.com/p/10lDn
Laurent Gbagbo anayeng'ang'ania madaraka Cote d'IvoirePicha: picture alliance/landov

Kulingana na azimio 1975, Laurent Gbagbo sharti aachie madaraka kadhalika anawekewa vikwazo vya usafiri na mali yake imezuiwa.Uamuzi huo umepitishwa wakati ambapo hali bado ni ya wasiwasi nchini Cote d'Ivoire.Ifahamike kuwa Alassane Ouatarra ndiye anayetambuliwa na jamii ya kimataifa kama mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka uliopita.

UN Sicherheitsrat Sitzung Flash-Galerie
Kikao cha Baraza la usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture alliance/landov

Azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,1975, linamshinikiza Laurent Gbagbo kuachia madaraka bila ya vikwazo vyovyote vile. Kadhalika, mwanasiasa huyo anayeng'ang'ania madaraka amewekewa vikwazo vya usafiri vitakavyowaathiri pia mkewe na washirika wake watatu wa karibu na mali yake itazuiliwa.Pindi baada ya azimio hilo kupitishwa Balozi wa Kudumu wa Nigeria katika Umoja wa Mataifa U.Joy Ugwu alisema kuwa nchi yake inaliunga mkono.

Azimio hilo linaviongezea makali vikwazo ambavyo vimekwa kama njia iliyokubaliwa ya kuutafutia suluhu mgogoro uliopo.Nigeria inaamini kuwa azimio hilo litafanikiwa kuupa nguvu zaidi wajibu wa ujumbe wa Umoja wa mataifa wa UNOCI unaowalinda raia wa Cote d'Ivoire.

Elfenbeinküste Wahl und Unruhen Flash-Galerie
Abidjan:Ghasia zahofiwa kusambaa katika mji mkuu baada ya Yamoussoukro kudhibitiwa na kambi ya OuattaraPicha: picture alliance/dpa

Yamoussoukro imetekwa nyara

Hatua hiyo imechukuliwa muda mfupi baada ya wapiganaji wanaomuunga mkono Alassane Ouattara kuudhibiti mji wa Yamoussoukro yaliko makao makuu ya serikali.Ghasia na purukushani za hivi karibuni nchini Cote d'Ivoire zimesababisha mauaji ya mamia ya watu.Ufaransa ndiyo iliyoliwasilisha pendekezo la azimio hilo kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.Kutokana na hali hiyo,balozi wake, Gerard Araud, ametahadharisha kuwa mapigano hayo huenda yakasambaa hadi mji mkuu wa Abidjan.Azimio hilo limeyalimulika mashambulio yanayowalenga raia wa kawaida ambayo huenda yakavitimiza vigezo vya kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na watuhumiwa kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa kivita ya ICC.Balozi wa kudumu wa Ufaransa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Gerard Araud  anaufafanua kuwa, ''Azimio hilo kwanza linasema kuwa Gbagbo lazima achie madaraka….linaeleza pia kuwa ujumbe wa UNOCI utayatimiza majukumu yake kwa kutumia mbinu zozote zile ili kuyazuwia matumizi ya silaha nzito mjini Abidjan,'' alisisitiza.

UNOCI na ulinzi wa raia

Ifahamike kuwa Umoja wa Mataifa una jumla ya wanajeshi alfu 11 wa kulinda amani wanaohudumu kwenye kikosi cha UNOCI.

Kwa upande mwengine, Umoja wa Afrika,Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, na mashirika mengine ya kimataifa yanamtambua Alassane Ouattara kama rais halali wa Cote d'Ivoire.Baadhi ya wawakilishi wa Baraza hilo la Usalama waliuelezea wasiwasi wao kuwa wajibu wa ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Cote d'Ivoire , UNOCI, huenda ukapindukia.Hata hivyo rasimu ya mwisho ya azimio hilo ilifahamisha kuwa ujumbe huo una wajibu wa kuzuwia matumizi yoyote yale ya silaha nzito.  

           

Youssoufou Bamba UNO Elfenbeinküste
Youssoufou Bamba,Balozi wa Cote d'Ivoire katika UNPicha: picture alliance/dpa

Mbinyo mkali zaidi?       

Kwa upande wao,mtazamo wa Shirika la Kutetea haki za binadamu Human Rights Watch unaripotiwa kueleza kuwa jamii ya kimataifa kamwe haijamuwekea Gbagbo mbinyo wa kutosha.Itakumbukwa kuwa kambi ya mwanasiasa huyo imetoa wito wa kusitisha mapigano,jambo lililopingwa na wafuasi wa hasimu yake Alassane Ouatarra.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinakadiria kuwa kiasi ya watu milioni moja wameyakimbia makazi yao tangu ghasia hizo zianze baada ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka uliopita.

Mwandishi: Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE

Mhariri:Aboubakary Liongo