1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yakubali kuongeza wanajeshi Somalia

Admin.WagnerD23 Desemba 2010

Baada ya kusitasita kwa muda mrefu, hatimaye jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuongeza idadi ya wanajeshi katika kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Afrika kilichoko Somalia, AMISOM.

https://p.dw.com/p/zojd
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: AP

Hadi sasa, kikosi cha AMISOM kilikuwa na wanajeshi 8,000. Na hapo jana (Jumatano, 21 Disemba 2010), Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likakubali pendekezo la Umoja wa Afrika, la kuongeza wanajeshi kwenye kikosi hicho. Uganda ndiyo ambayo itatoa wanajeshi 4,000 wa ziada; na sasa kuifanya idadi kamili kuwa wanajeshi 12,000.

Wanadiplomasia katika Baraza la Usalama, wanasema kwamba, kuongezwa kwa wanajeshi hao, kutaiwezesha AMISOM kuikamata tena Mogadishu kutoka mikononi mwa wanamgambo wa Al-Shabaab, ambao wanashikilia sehemu kubwa ya Somalia.

Azimio hilo la jana (Jumatano, 21 Disemba 2010), la Baraza la Usalama, linamuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, kutoa vifaa na huduma kwa AMISOM. Vile vile linawataka wanachama wa Umoja huo na jumuiya za kimataifa, kuchangia kwenye mfuko maalum wa AMISOM, unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Uganda ndiyo nchi yenye wanajeshi wengi zaidi katika kikosi cha AMISOM. Balozi wake kwenye Umoja wa Mataifa, Ruhakana Rugunda, aliliambia Baraza la Usalama kwamba azimio hili litaongeza uwezo wa AMISOM kutekeleza majukumu yake, lakini akasema ni "jambo la muhimu kwa kikosi cha AMISOM kupata nyenzo zote zinazohitajika na kwa wakati."

Rugunda aliitaka serikali ya Somalia kuendelea kuwa madhubuti; na kuendeleza juhudi zake za kukutana na makundi ya upinzani, ambayo yako tayari kushirikiana nayo kwa kile alichokiita: "moyo wa kujenga mashirikiano na mapatano."

Kimsingi hasa, nchi za Afrika zilikuwa zikilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kupeleka kikosi kamili cha Umoja huo nchini Somalia ili kuchukua nafasi ya AMISOM, lakini Baraza hilo limekuwa likisema kwamba, litafanya hivyo, pale tu hali ya usalama itakapokuwa imeimarika.

Ni baada ya kushindwa kwa pendekezo hilo la mwanzo, ndipo Umoja wa Afrika ukapeleka pendekezo la kutaka kikosi cha AMISOM kiwe na wanajeshi 20,000, lakini nalo pia likapingwa na mataifa makubwa kwenye Baraza la Usalama, kwa madai kuwa idadi hiyo ni kubwa mno.

Sehemu kubwa ya idadi ya wanajeshi 12,000 iliyoridhiwa sasa na Baraza hilo, inatoka Uganda na Burundi. Sehemu kubwa pia ya gharama za AMISOM, hutolewa na jumuiya ya kimataifa. Tayari kikosi hiki kinapokea kiasi ya dola za Kimarekani milioni 130 kwa mwaka kutoka Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/REUTERS

Mhariri: Josephat Charo