1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watoa misaada zaidi ya 100 wauawa Sudan Kusini

20 Julai 2018

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, limearifu hii leo kwamba zaidi ya wafanyakazi 100 wa misaada ya kiutu wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini tangu kuzuka kwa vita hivyo mwaka 2013.

https://p.dw.com/p/31phV
Süd-Sudan Hilfslieferungen wegen Dürre
Picha: REUTERS

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, limearifu hii leo kwamba zaidi ya wafanyakazi 100 wa misaada ya kiutu wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini tangu kuzuka kwa vita hivyo mwaka 2013, wakati  mkutano uliokutanisha wanachama wa baraza hilo na baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika, nao ukisema hali nchini humo ni ya kutia wasiwasi. 

Taarifa ya pamoja ilibainisha kwamba wafanyakazi 107 wa misaada ya kiutu walikufa katika mzozo huo, ambao ulianza miaka miwili baada ya Sudan Kusini kupata uhuru wake. Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika walikutana mjini New York kwa ajili ya mkutano wa mwaka kujadili mzozo wa sasa pamoja na ufadhili.

Vita hivyo vilizuka baada ya rais Salva Kiir kumtuhumu kiongozi wa upinzani Rieck Machar, ambaye alikuwa makamu wake kwa kupanga njama ya mapinduzi. Tangu wakati huo maelfu ya raia wameuawa, na takriban Wasudan Kusini milioni 4 wameyakimbia makazi yao.

Ethnische Unruhen in Süd-Sudan
Watu milioni nne wanaripotiwa kuyahama makazi yao kutokana na vita nchini Sudan KusiniPicha: DW

Wakati kukitolewa taarifa hii, mwenyekiti wa baraza la usalama la Umoja wa Afrika, Sebade Toba amesema kwenye mkutano uliowakutanisha wanachama wa baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa na wanachama wa baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, AUPSC kuwa hali ilivyo nchini Sudan Kusini ni ya kutia wasiwasi mkubwa.

Amesema, watu bado wanaendelea kukabiliwa na mateso, na hali ya kiutu ni ngumu mno na imekuwa changamoto kubwa kwao, ingawa amesifu juhudi zinazochukuliwa za kusaka suluhu ya mzozo huo.

Balozi wa Sweden katika Umoja wa Mataifa, Olog Skoog amenukuliwa akisema kwamba changamoto zinazowakabili katika suala la usalama na maendeleo kwa kiasi kikubwa zinafanana, hivyo mataifa ya Afrika yanapokabiliana nazo, hufanya hivyo kwa niaba yao.

Mabaraza hayo ya usalama yamekuwa yakifanya mikutano ya pamoja ya mwaka tangu mwaka 2007 kwa kupokezana, ama katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York au makao makuu ya Umoja wa Afrika, yaliyopo Addis Ababa. Matamko ya pamoja kwa kawaida hutolewa baada ya mikutano hiyo ya mwaka. 

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga