1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Haki za binadamuAfghanistan

UN waitaka Taliban kuondoa sheria zinazokandamiza wanawake

27 Februari 2024

Zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wameutaka utawala wa Taliban kuondoa sheria zote zinazokandamiza na kuwabagua wanawake na wasichana.

https://p.dw.com/p/4cv47
Wanawake wa Afghanistan wakifanya maandamano ya kudai haki zao mjini Kabul
Wanawake wa Afghanistan wakifanya maandamano ya kudai haki zao mjini KabulPicha: AFP/Getty Images

Sheria hizo ni pamoja na kupiga marufuku elimu ya wasichana na haki ya wanawake kufanya kazi na kutembea kwa uhuru.

Taarifa ya wajumbe 11 kati ya 15 wa baraza hilo la Umoja wa Mataifa imelaani ukandamizaji wa Taliban kwa wanawake na wasichana tangu walipoingia madarakani mnamo Agosti mwaka 2021.

Wajumbe hao pia wamehimiza ushiriki wa wanawake katika masuala mbalimbali ya umma, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii hasa katika ngazi ya kufanya maamuzi.

Wawakilishi wa mashirika ya kiraia ya Afghanistan, wakiwemo wanawake walishiriki katika mkutano huo uliofanyika mjini Doha, Qatar japo Taliban walikataa kuhudhuria.

Utawala wa Taliban haujatambuliwa na nchi yoyote huku mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan akiwaonya viongozi hao kuwa, utawala huo kamwe hautatambuliwa kimataifa hadi watakapoondoa sheria zinazokandamiza na kuwabagua wanawake na wasichana.