1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

UN: Vita Sudan vyasababisha vifo vya takriban watu 9,000

16 Oktoba 2023

(Miezi sita ya vita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha RSF imesababisha vifo vya takriban watu 9,000 na mojawapo ya hali ngumu zaidi ya misaada ya kibinadamu katika historia ya hivi karibuni

https://p.dw.com/p/4XZtp
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura - Martin Griffiths akizungumza na wanahabari kabla ya mkutano wa wafadhili wa mzozo wa kibiadamu nchini Yemen akiwa Geneva mnamo Februari 27,2023
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura - Martin GriffithsPicha: Fabrice Coffrini/AFP

Sudan imekumbwa na machafuko tangu katikati ya mwezi wa Aprili, wakati mvutano kati ya mkuu wa jeshi la nchi hiyo Jenerali Abdel-Fattah Burhan na kamanda wa Kikosi cha RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ulipogeuka na kuwa vita vya wazi. Katika taarifa ya maadhimisho ya miezi hiyo sita tangu kuzuka kwa vita hivyo, Griffiths amesema raia wa nchi hiyo hawajapata nafuu kutokana na umwagaji damu na hali ya hofu. Griffiths ameongeza kuwa ripoti za kutisha kuhusu ubakaji na uhalifu wa kingono zinaendelea kuibuka.

Mapigano yasababisha mamilioni ya watu kutorokea nchi jirani

Awali mapigano hayo yalikuwa yamejikita mjini Khartoum lakini kwa haraka yakaenea katika maeneo mengine kote nchini humo pamoja na eneo la Magharibi la Darfur ambalo tayari lilikuwa limekumbwa na machafuko. Griffiths anasema mapigano hayo yanaripotiwa kusababisha mauaji ya watu hao elfu 90 na kuwalizimisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao aidha kuelekea katika maeneo salama ndani ya Sudan ama  kutorokea nchi Jirani.

Soma pia:UN: Mashambulizi ya kikabala yasababisha vifo vya mamia Darfur

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa, ameongeza kuwa mzozo huo ulisababisha kusambaratika kwa jamii, huku watu wasiojiweza wakikosa njia ya kupata msaada wa kuokoa maisha yao na pia kuongeza mahitaji ya msaada wa kibinadamu katika mataifa jirani walikotorokea mamilioni ya watu.

Wakazi wa Darfur waliotoroka vita wapanda malori ya Umoja wa Mataifa kuwasafirisha katika maeneo salama ya kambi za wakimbizi mjini Ourang, viungani mwa Adre, Chad mnamo Julai 25, 2023
Wakazi wa Darfur waliotoroka vita wapanda malori ya Umoja wa Mataifa kuwasafirisha katika maeneo salama Picha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

 Mapigano yamewaacha watu milioni 25, wakihitaji misaada ya kibinaadamu.

Kulingana na Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM), zaidi ya watu milioni 4.5 wamekuwa wahamiaji wa ndani nchini Sudan, huku wengine zaidi ya milioni 1.2 wakikimbilia nchi jirani. Griffiths amesema pia mapigano hayo yamewaacha watu milioni 25, hii ikiwa zaidi ya nusu ya idadi jumla ya Wasudan wakihitaji misaada ya kibinaadamu.

Soma pia: Karibu watoto 500 wamefariki kutokana na njaa Sudan

Kuongezea maafa hayo, mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliripotiwa katika mji mkuu na maeneo mengine nchini humo, huku zaidi ya visa 1,000 vinavyoshukiwa kuwa vya maambukizi ya ugonjwa huo vikigunduliwa mjini Khartoum na katika mikoa ya Kordofan na Qadarif.

Tangu kuzuka kwa vita hivyo, eneo kubwa la Khartoum linalojumuisha miji ya Khartoum, Omdurman na Khartoum Kaskazini imekuwa uwanja wa vita, huku mashambulizi ya anga na makombora yakifanyika katika maeneo yenye watu wengi.

Soma pia: Shambulio la anga lawaua raia 20 huko Sudan

Ukatili wa hivi majuzi huko Darfur ulichochea mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kutangaza mwezi Julai kuwa anachunguza madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika mapigano ya hivi karibuni katika eneo hilo.