1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mafuriko Sudan Kusini yataleta utapia mlo mwakani

7 Novemba 2023

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, limetahadharisha zaidi ya watoto milioni 1.6 walio chini ya umri wa miaka mitano watakabiliwa na utapiamlo mwaka ujao nchini Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/4YVcn
Faharasa ya Njaa Duniani | Wanawake Sudan Kusini wakisubiri mlo katika kituo cha kugawa chakula
Wanawake Sudan Kusini wakisubiri mlo katika kituo cha kugawa chakula Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Hii ni kufuatia kuongezeka kwa magonjwa ya mripuko kutokana na mafuriko.

Mary-Ellen McGroarty, mkurugenzi wa WFP huko Juba amesema huu ndio uhalisia wa kuishi na athari za mgogoro wa hali ya hewa na kwamba kumeshuhudiwa ongezeko la utapiamlo ambalo amesema ni matokeo ya moja kwa moja ya kuishi katika hali ya msongamano wa watu na mafuriko.

Sudan Kusini, ni taifa jipya zaidi duniani ambalo limekumbwa na mizozo mikali, majanga ya asili, kuzorota kwa uchumi na migogoro ya kisiasa tangu lilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Sudan mnamo mwaka 2011.

Ni moja ya mataifa maskini zaidi duniani na lililokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka mitano na kusababisha vifo vya takriban watu 380,000.