1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mabilioni yanahitajika kuzisaidia nchi masikini

8 Mei 2020

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa serikali, kampuni na matajiri duniani kuchangia dola bilioni 6.7 kusaidia mataifa masikini kupambana na virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3bvCn
Coronavirus Südafrika Johannesburg Essensausgabe
Picha: AFP/L. Sola

Akizungumza wakati wa mkutano wa kutoa wito mpya kwa ulimwengu kuchangia fedha kuzisaidia nchi masikini, mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amesema mataifa yenye uwezo duni yanakabiliwa na kitisho maradufu cha athari za virusi vya corona.

Lockcock ameonya kuwa kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha janga la njaa, machafuko na mizozo zaidi. 

Lowcock amesema ugonjwa wa COVID-19 tayari umeathiri kila nchi na kila mtu duniani na kilele cha janga hilo kinatarajiwa kuleta mtikisiko kwa mataifa masikini kwa muda wa miezi mitatu hadi sita inayokuja.

Amesema ombi la awali la Umoja wa Mataifa la dola bilioni 2 limeongezeka kwa sababu ushahidi unaonesha watu wengi wanapoteza kipato, hakuna nafasi za kazi, bei za vyakula zimepanda na watoto wanakosa chanjo na matibabu muhimu.

Mwanadiploamasia hiyo amesisitiza nchi masikini zinazongwa na athari za kiafya zinazotokana na janga la corona, matokeo ya kudorora kwa uchumi wa dunia pamoja na vizuizi vikali vya shughuli za uchumi vinavyowekwa kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

Guterres asema msaada unahitajika sasa

Die schweizerische Vizepräsidentin Simonetta Sommaruga, die schwedische Außenministerin Margot Wallström, der Generalsekretär der Vereinten Nationen, Antonio Guterres, und der Vize-Generalsekretär der Vereinten Nationen für humanitäre Angelegenheiten und Nothilfekoordinator Mark Lowcock
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Getty Images/F. Coffrini

Wakati wa mkutano huo kwa njia ya video Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametilia mkazo umuhimu wa kupatikana kiwango hicho cha fedha.

"Tunahitaji dola bilioni 6.7 kuwalinda mamilioni ya watu na kusaidia kuzuia virusi hivi kusambaa tena kote duniani. Iwapo COVID-19 itasababisha maafa kwenye maeneo masikini sote tuko kwenye hatari. Ninatoa rai ya uungaji wenu  mkono katika ombi hili" amesema Guterres.

Kwenye mkutano huo mkurugenzi wa mpango wa chakula wa Umoja wa Mataifa David Beasley amesema njia pekee ya kuwaepusha na janga la njaa kiasi watu milioni 265 duniani na kutoa fedha na kuhakikisha usambazaji wa vyakula hautatiziki.

Beasley ameonya ikiwa vijana walio mijini watapoteza ajira na kukosa chakula, kutashuhudia, maandamano, migomo na kukosekana utulivu masuala yatakayoigharimu zaidi dunia kutoa msaada hivi sasa.

Kiwango kilichopatikana bado ni kidogo 

Schweiz | UN-Nothilfekoordinator Mark Lowcock | Klimawandel | Migration
Mratibu wa Misaada ya Kiutu wa Umoja wa Mataifa, Mark lowcockPicha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Hadi sasa Umoja wa Mataifa umekusanya kiasi dola bilioni 1 kutoka ombi la awali la dola bilioni mbili na wachangiaji wakubwa ni mataifa ya Ulaya, Japan, nchi za ghuba pamoja na Canada.

Wito mpya wa kuchangisha dola bilioni 6.7 utajumuisha mataifa mengine 9 masikini katika orodha ya mataifa 54 yaliyoorodheshwa katika mpango wa awali.

Hayo yanajiri wakati Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limeonya kuwa kiasi watu 190,000 wanaweza kufa barani Afrika katika mwaka wa kwanza wa janga la COVID-19 iwapo hatua za udhibiti zitashindwa kufa nya kazi.

Taarifa ya WHO imetokana na ripoti ya tathmini na makadirio ya vifo iliyojumuisha mataifa 47 ya Afrika yenye jumla ya watu bilioni 1.

Masuala kama miundombinu duni, viwango vya juu vya umaskini na mizozo ndiyo itachangia kwa sehemu kubwa idadi hiyo kubwa ya vifo.