1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kuandaa mkutano wa Kimataifa wa kuyalinda maeneo takatifu

22 Januari 2021

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalopinga uharibifu wa maeneo ya kuabudu na kumtaka Katibu Mkuu wa Umoja huo kuandaa mkutano wenye lengo la kuhamasisha umma juu ya kuheshimu na kuyalinda maeneo hayo

https://p.dw.com/p/3oHCA
Jerusalem Ostern Coronavirus Covid-19 Ausgangssperre
Picha: Getty Images/

Azimio hilo lililopitishwa jana Alhamisi linapinga kulengwa kwa maeneo ya kitamaduni ikiwemo maeneo ya kuabudu, na vifaa vinavyofanyiwa matambiko.

Kushambuliwa kwa maeneo hayo kunasemekana kufanywa na magaidi pamoja na wanamgambo hali inayosababisha kuharibiwa vibaya kwa sehemu hizi takatifu na hata kuibwa kwa vitu vilivyoko ndani na kuuzwa kiharamu.

Azimio hilo linalopinga kabisa mashambulizi yote katika maeneo ya kuabudu, pamoja na madhabahu lilipendekezwa na Saudi Arabia na kuungwa mkono na mataifa ya Kiarabu ikiwemo Misri, Iraq, Jordan, Kuwait, Yemen, Bahrain, Sudan, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu na Palestina inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa kama nchi mwangalizi, isiyo mwanachama wake.

Bangladesh, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Equatorial Guinea, Mauritania, Morocco, Nigeria, Pakistan, Ufilipino na Venezuela pia zilikuwa miongoni mwa mataifa yaliounga mkono azimio hilo. Marekani na Umoja wa Ulaya pia waliliunga mkono azimio hilo.

Kingine inachoeleza azimio hilo ni kutambua kuwa haki, uhuru wa mawazo pamoja na dini ni mambo yaliyo katika mkataba wa Umoja wa Mataifa unaosimamia haki za binaadamu na kutambua juhudi za awali za kimataifa zilizozingatia kuzuwia uharibifu wa maeneo ya kuabudu.

Sehemu takatifu zina historia inayopaswa kulindwa

Indien Urteil Moschee
Maafisa wa Usalama wakishika doria nje ya msikiti mmoja nchini IndiaPicha: Reuters/P. Waydance

Maeneo hayo yanawakilisha historia, kutambua jamii fulani na tamaduni za watu wa kila nchi duniani na ni lazima yaheshimiwe na kulindwa wakati wote ama kwenye vita au katika mashambulizi ya kigaidi.

Kwa sasa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameombwa kuitisha mkutano wa kimataifa utakaoyajumuisha mashirika ya umoja huo, nchi wanachama 193 wanaounda Umoja wa Mataifa, wanasiasa, viongozi wa kidini, vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na wengine ili kutekeleza mpango wa umoja huo wa kuheshimu na kuyalinda maeneo ya kuabudu.

Katika Mpango huo uliotolewa mwezi Septemba mwaka 2019, uligusia ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi, Waislamu, mashambulizi dhidi ya Wakristo na migogoro inayowalenga wanachama wa dini tofauti pamoja na tamaduni zao.

Mpango huo unaangazia namna tofauti ya kuzuwia mashambulizi kama hayo na utayari wa kuwa na majibu sahihi yanayoleta maridhiano na kutaka serikali kutangaza wazi kuheshimiwa na kulindwa kwa maeneo matakatifu.

Chanzo: ap,reuters