1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN: Israel na Hamas wanatenda uhalifu wa kivita

27 Oktoba 2023

Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imezishutumu Ijumaa Israel na Hamas kuwa zimetenda uhalifu wa kivita. uhalifu huo ni kitendo cha Israel kuuzingira na kuweka vikwazo huko Gaza, na ukatili wa kundi la Hamas.

https://p.dw.com/p/4Y7Wy
UN Ravina Shamdasani
Msemaji wa Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani, akizungumza mnamo Julai 11,2014 na wanahabari mjini Geneva, Uswisi kufuatia mashambulizi ya Israel huko Gaza. Picha: Fatih Erel/AA/picture alliance

Msemaji wa Ofisi hiyo ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani, amesema siku ya Ijumaa huko mjini Geneva, Uswisi, kuwa adhabu ya jumla dhidi ya Wapalestina ni uhalifu wa kivita huku akitaka hilo likomeshwe mara moja.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa  limesema pia kuwa kundi la wanamgambo wa Kiislamu wa Palestina la Hamas lilifanya uhalifu wa kivita na ukatili mwingine ikiwa ni pamoja na utekaji nyara wa raia kutoka Israel wakati wa mashambulizi mabaya ya Oktoba 7. Shamdasani ameyataka makundi ya Kipalestina kusitisha "mashambulizi ya kiholela" dhidi ya Israel.

Maafisa wa Hamas ziarani Urusi

Urusi imeutetea hii leo uamuzi wake wa kuualika ujumbe wa kundi la Hamas mjini Moscow, ikisema kuna ulazima wa kudumisha mawasiliano na pande zote katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

Israel imeukosoa uamuzi huo na kuutaja kuwa wa kusikitisha na kuihimiza Moscow kuwafukuza wajumbe hao wa Hamas. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema ujumbe huo ulikutana na wawakilishi wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi na sio na  Rais Vladimir Putin  au maafisa wa Kremlin na kusema wataendelea pia mazungumzo na Israel.

Musa Abu Marsuk (2019)
Afisa mwandamizi wa Hamas, Mousa Mohammed Abu Marzouk(Picha ya Februari 12,2019)Picha: Sefa Karacan/AA/picture alliance

Urusi imedumisha mahusiano na wadau wote muhimu huko Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na Israel, Iran, Syria, Hamas, na hata Mamlaka ya Palestina inayoungwa mkono na Mataifa ya Magharibi. Lakini kuhusiana na mzozo huu kati ya Israel na Palestina, Urusi imekuwa ikiitupia lawama Marekani na kusema imefeli kidiplomasia.

Ubalozi wa Urusi nchini Israel umetoa taarifa inayorejelea wito wa Moscow wa kutaka kuwepo mara moja usitishwaji mapigano, kuachiwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas na kuruhusu misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza.

Soma pia: Israel yafanya shambulio jingine Ukanda wa Gaza

Shirika la habari la Urusi TASS limeripoti leo Ijumaa kuwa afisa mwandamizi wa Hamas, Abu Marzouk, amefanya mazungumzo mjini Moscow na naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran, Ali Baghiri Kani.

Aidha Urusi imesisitiza pia kwamba hakuna uwezekano wowote wa taifa hilo kuingizwa katika vita hivyo lakini imekemea mashambulizi ya kulipiza kisasi ya jeshi la Marekani huko Syria ambayo yaliwalenga wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, na kusema inaweza kuchochea mzozo huo kuenea katika ukanda mzima.

Madaktari wa ICRC wawasili Gaza

Gaza Stadt | Fahrzeug des roten Kreuz
Gari ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC ikiwasafirisha Wapalestina wa huko Gaza ambao nyumba zao zimeharibiwa na mashambulizi ya jeshi la Israel: 13.10.2023Picha: Ashraf Amra/AA/picture alliance

Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita hivyo, madaktari wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, wamewasili Gaza leo Ijumaa, wakipitia kwenye kivuko cha Rafah pamoja na wataalamu wengine wanne wa ICRC na malori sita ya misaada. Mkurugenzi shirika hilo katika ukanda huo, Fabrizio Carboni, amesema msafara huo ni "msaada mdogo unaoleta matumani lakini hautoshi".

Soma pia: UN yasema msaada usio na kikomo unahitajika Gaza

Israel imeapa kuliangamiza kundi la Hamas na imekuwa ikiendesha mashambulizi makubwa ya kulipiza kisasi baada ya shambulio la Oktoba 7 ambapo wanamgambo hao wa Kipalestina waliwaua watu 1,400 na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 200, kwa mujibu wa Tel Aviv.

Kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), watu wenye ulemavu huko Gaza wanateseka zaidi kutokana na mashambulizi ya makombora ya Israel huku wakilazimika pia kuhamishwa. Wizara ya Afya huko Gaza na mashirika ya kimataifa yamesema hadi sasa  Wapalestina 7,326 wameuawa huku 3038 wakiwa ni watoto.