1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: IS ina hadi wapiganaji 30,000 Iraq na Syria

14 Agosti 2018

Umoja wa Mataifa umesema kati ya wapiganaji 20,000 hadi 30,000 wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS bado wako Iraq na Syria, licha ya kundi hilo la jihadi kushindwa na kusitisha kuwasajili wapiganaji wa kigeni.

https://p.dw.com/p/337zg
Symbolbild Rakka Kämpfer der IS
Picha: picture-alliance/dpa

Ripoti iliyotolewa jana na timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaosimamia vikwazo imeeleza kuwa wapiganaji hao wataendelea kuwepo kwenye nchi hizo, huku wakisaidiwa kwa kiasi kikubwa na wafuasi wao walioko nchini Afghanistan, Libya, Kusini mashariki mwa Asia na Afrika Magharibi na kwamba mtandao huo wa kimataifa wa IS ni kitisho kikubwa kama ilivyo kwa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wengi wa viongozi muhimu wa IS wanaendelea kuhamishiwa Afghanistan, ambako kundi hilo lina wapiganaji kati ya 3,500 na 4,000 na imeelezwa kuwa idadi hiyo inaongezeka. Ripoti hiyo ya wataalamu wanaochunguza vikwazo dhidi ya IS na Al-Qaeda ambayo imewasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inakadiria kuwa idadi ya sasa ya wafuasi wa IS nchini Iraq na Syria wametoka katika serikali ambazo hawajazitaja.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mtandao wa Al-Qaeda pia unaendelea kuonyesha uwepo na ujasiri wake pamoja na washirika wake kwa kiasi kikubwa kuliko IS katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Somalia, Yemen, Asia Kusini na kanda ya Sahel barani Afrika. Wataalamu hao wanasema kuwa viongozi wa Al-Qaeda nchini Iran wameendelea kupata umaarufu zaidi na wamekuwa wakifanya kazi pamoja na kiongozi mkuu wa mtandao huo, Ayman al-Zawahri, ambaye ameelezea kufanikiwa zaidi kuliko awali, ikiwemo katika matukio ya Syria.

Aiman az-Zawahiri Videobotschaft
Kiongozi wa Al-Qaeda, Ayman al-ZawahriPicha: Reuters/SITE

Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, wapiganaji wachache wa kigeni waliondoka Iraq na Syria kuliko ilivyotarajiwa, baada ya jeshi kulisambaratisha kundi hilo. Iraq ilijitangazia ushindi dhidi ya IS mwezi Desemba, na kufanikiwa kuyakomboa maeneo yote yaliyokuwa yakidhibitiwa na wapiganaji hao wenye itikadi kali tangu mwaka 2014. Ushindi huo ulifanikiwa kwa msaada wa muungano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani.

Ingawa wapiganaji wengi wa IS, wanamipango na makamanda waliuawa katika mapigano na wapiganaji wengine na wafuasi wamekimbia katika maeneo ya mapambano, bado kuna wapiganaji ambao wamejificha kwenye jamii zinazohitaji msaada pamoja na maeneo ya mijini.

Wakati kiwango cha mashambulizi ya kigaidi kikiwa kimepungua barani Ulaya, wataalamu wanasema baadhi ya serikali zinatathmini kwamba wanaopanga ugaidi chini kwa chini wote bado wako na pengine zaidi ya ilivyokuwa awali.

IS ina wafuasi 250 hadi 500 nchini Yemen, ikilinganishwa na wapiganaji kati ya 6,000 na 7,000 wa Al-Qaeda. Katika ukanda wa Sahel, IS inaendesha zaidi shughuli zake katika mpaka wa Mali na Niger, lakini ina wafuasi wachache ikilinganishwa na kundi la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslim, JMIN linalofungamana na Al-Qaeda.

Aidha, kundi la kigaidi la Al-Shabaab linalofungamana na Al-Qaeda limetawala nchini Somalia, lakini kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, kundi la IS lina mkakati wa kujitanua kwenye maeneo ya katikati na kusini mwa Somalia. Ripoti hiyo inafafanua kuwa baadhi ya wapiganaji wa IS wanaweza wakaamua kuhamia katika jimbo la Puntland.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, DPA, AFP
Mhariri: Josephat Charo