1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waunga mkono maandamano Marekani

2 Juni 2020

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel amesema kifo cha George Floyd kilikuwa matokeo ya matumizi mabaya ya mdaraka, na kwamba kanda hiyo ya mataifa 27 wanachama imeshtushwa na kuhuzunishwa nacho.

https://p.dw.com/p/3d9Xc
Brüssel Belgien Josep Borrell
Picha: picture-alliance/dpa/European Council/Zucchi-Enzo

Kamishna mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel amewaambia waandishi habari kwamba kama ilivyo kwa watu nchini Marekani, umoja huo pia umeshtushwa na kifo cha George Floyd, kilichotokana na kukandamizwa shingoni kwa goti na askari polisi mweupe kwa muda wa zaidi ya dakika nane hadi alipoacha kupumua.

Borrel amesema maafisa wanaosimamia utekelezaji wa sheria hawapaswi kutumia uwezo wao kwa namna iliyotumiwa katika kifo cha kuhuzunisha cha Floyd, na kuongeza kuwa hayo ni matumizi mabaya ya madaraka yanayopaswa kulaaniwa.

"Tunaunga mkono haki ya kuandamana kwa amani na pia tunalaani vurugu na ubaguzi wa rangi wa aina yoyote na kwa uhakika tunatoa wito wa kupunguza hali ya wasiwasi," amesema Borrell na kuongeza kuwa, "tuna imani na uwezo wa Wamarekani kuja pamoja, kutibu majeraha na kushughulikia masuala haya muhimu wakati huu mgumu na naomba nirudie kwamba maisha ya watu wote ni muhimu, maisha ya watu weusi pia ni muhimu."

Deutschland Berlin | Heiko Maas, Bundesaußenminister
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas, amesema maandamano ya Marekani ni zaidi ya halali.Picha: Reuters/F. Bensch

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas, amesema katika mkutano na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba, kwamba George Floyd aliuawa kikatili na kwamba maandamano yanayoendelea Marekani yanaeleweka na ni zaidi ya halali.

Maas ameepuka kuilaumu moja kwa moja serikali ya Marekani kwa namna ilivyoshughulikia maandamano hayo na ukandamizaji wa polisi dhidi ya washiriki wa maandamano hayo, akisema kila kitendo cha vurugu kinapaswa kuchunguzwa, na kwamba waandishi habari wanapaswa kuruhusiwa kufanyakazi kwa uhuru.

Maandamano ya mshikamano yanaendelea kufanyika katika miji mengine duniani, kama vile Sydney, ambako waandamanaji wamekuwa wakirudia maneno ya "siwezi kupumua" baadhi ya maneno ya mwisho aliyoyasema Floyd na David Dungay, mwanaume wa kabila la asili la Aborigin mwenye umri wa miaka 26, aliyefariki katika gereza mjini Sydney mwaka 2015, wakati akizuwiwa na walinzi watano wa gereza.

Viongozi wa Afrika wazidi kupaza sauti

Wakati huo huo, viongozi zaidi wa Kiafrika wanazidi kupaza sauti kuhusiana na kifo cha Floyd. Rais wa Ghana Nana Akufo-Ado, amesema katika taarifa kwamba haiwezi kuwa sahihi katika karne hii ya 21, kwamba taifa kubwa la kidemokrasia kama Marekani, linaendelea kupambana na tatizo la ubaguzi wa kimfumo.

Ghanas Präsident Nana Akufo-Addo
Rais wa Ghana Nana Akufo-Ado amesema hakutarajia kwamba mauaji ya kikatili yanaweza kuwa yanatokea katika Marekani ya karne ya 21.Picha: picture alliance/dpa/AP Photo/G. V. Wijngaert

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ameomba sala, ya kuwepo na haki na uhuru kwa watu wote wanaopaita Marekani kuwa ni nyumbani.

Waziri wa fedha wa Afrika Kusini Tito Mboweni, amekumbuka kuongoza kundi dogo la waandamanaji nje ya ubalozi wa Marekani miaka kadhaa iliyopita kupinga mauaji ya dhahiri ya watu weusi. Mboweni amesema balozi wa Marekani wakati huo, Patrick Gaspard, alimualika ofisini kwake na kumuambia kwamba "unachokiona si chochote, hali ni mbaya zaidi."

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam amehoji ukosoaji wa kigeni kuhusiana na sheria mpya ya usalama inayoanzishwa katika eneo hilo la China lenye uhuru wake wa ndani, akisema Wamarekani wanachukulia usalama wao wa ndani kwa uzito, lakini kwa usalama wa nchi yake na hasa Hong Kong, wanautazama kwa mbali.

Chanzo: Mashirika