1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya washindwa kukubaliana mkutano na Putin

25 Juni 2021

Umoja wa Ulaya umelikataa pendekezo la Ujerumani na Ufaransa la kurejesha mikutano na Rais Vladimir Putin wa Urusi baada ya upinzani mkali wa mataifa wanachama yanayotiwa wasiwasi na "uchokozi wa Urusi."

https://p.dw.com/p/3vXmq
EU Gipfel Deutschland Österreich Merkel Kurz
Picha: Olivier Matthys/AP Photo/picture alliance

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa kilele mjini Brussels usiku wa kuamkia Ijumaa (25 Juni), Kansela Angela Merkel alisema walichukuwa muda mrefu kulijadili pendekezo hilo kwa kina, lakini hatimaye hawakufikia muafaka.

"Haikuwezekana kukubaliana leo lakini kwangu la muhimu ni kwamba mfumo wa majadiliano unakuwepo na tunaufanyia kazi. Nilitamani tungepiga hatua kubwa zaidi ya hii, lakini inatosha hivi ilivyo na tutaendelea kulishughulikia suala hili." Alisema kiongozi huyo wa Ujerumani ambaye huu ni mkutano wake wa mwisho wa kilele kabla ya kustaafu mwezi Septemba.

Ujerumani na Ufaransa, kwa pamoja, zilikuwa zimechomeka pendekezo hilo kwenye ajenda za mkutano huo wa kilele zikitaka yawepo mazungumzo kama yale ya Rais Joe Biden wa Marekani na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, mjini Geneva wiki iliyopita.

Lakini pendekezo hilo lilikumbana na upinzani mkali kutoka mataifa wanachama - hasa ya Ulaya Mashariki - ambayo yalisema "kuinyooshea Urusi mkono wa mazungumzo kabla ya kubadilisha mtazamo wake ni kosa kubwa."

Ukraine yakataa katakata

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alikuwa wa mwanzo kukosowa pendekezo hilo aliloliita "ukiukwaji wa hatari wa sera ya vikwazo ya Umoja wa Ulaya."

Brüssel EU Gipfel | Merkel
Kansela Angela Merkel ameshindwa kuwashawishi wenzake kwenye Umoja wa Ulaya kuwa na mkutano wa kilele na Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: John Thys/REUTERS

Rais wa Lithuania, Gitanas Nauseda, alisema kwamba upande wake haoni kwamba kutakuwa na mkutano wowote kati ya viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na Urusi, akielezea jinsi mahusiano ya pande hizo mbili yanavyozidi kuzoroteshwa na kile alichodai ni "tabia mbaya ya Urusi."

Kukataliwa kwa pendekezo hili la Ujerumani na Ufaransa, ambalo lilisifiwa hapo jana na Ikulu ya Kremlin iliyosema kuwa Rais Putin ni "muungaji mkono moja kwa moja", kumeikasirisha sana Urusi.

Masaa machache baada ya uamuzio huo kutangazwa, wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo ilisema kitendo hicho kinaashiria jinsi Umoja wa Ulaya ulivyotwaliwa mateka na mataifa machache wanachama. 

Laiti pendekezo hilo lingepita, huenda Urusi ingelipata fursa ya kushawishi kuondolewa baadhi ya vikwazo ilivyowekewa na Umoja wa Ulaya baada ya hatua yake ya kulitwaa jimbo la Crimea kutoka Ukraine.

Mkutano wa mwisho wa kilele baina ya pande hizo mbili ulifanyika mwaka 2014, na tangu hapo Rais Putin amekuwa akikutana tu na kiongozi mmoja mmoja kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya katika matukio machache sana.