1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Umoja wa Ulaya wapanga kuiwekea vikwazo vipya Urusi

2 Februari 2023

Umoja wa Ulaya unapanga kuiwekea vikwazo vipya Urusi, wakati maadhimisho ya kukumbuka mwaka mmoja tangu taifa hilo lilipoivamia Ukraine yakikaribia

https://p.dw.com/p/4N1mH
Ukraine, Kiew | Von der Leyen trifft Selenskyj
Picha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout/REUTERS

Akiwa ameongozana na mwenyeji wake, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kyiv mapema Alhamis, Rais wa Halmashauri ya Umoja huo Ursula von der Leyen amesema kwa pamoja na washirika wao wa kundi la G7, wataimarisha zaidi vikwazo dhidi ya Urusi.

"Hii leo Urusi inapitia wakati mgumu sana kutokana na vikwazo tulivyoiwekea na vinavyoathiri uchumi wake. Ukomo wa bei kwenye bidhaa za mafuta ghafi unaigharimu Urusi karibu yuro milioni 160 kwa siku na tutazidi kuiongezea shinikizo. Sisi na washirika wetu wa G7 tutatangaza bei nyingine za ukomo kwenye bidhaa za mafuta za Urusi na itakapofika Februari 24, mwaka mmoja tangu ilipoivamia Ukraine, tunalenga kutangaza awamu ya kumi ya vikwazo," alisema Von der Leyen.

Rais wa Halmashauri ya Umoja huo Ursula von der Leyen amesifu juhudi zinazofanywa na Ukraine kukabiliana na ufisadi, wakati ikiendelea na kuwachunguza maafisa wake wa ngazi za juu wanaohusika na matumizi mabaya ya mali ya umma. 

Ukraine, Kiew | Von der Leyen trifft Selenskyj
Rais wa Halmashauri ya Umoja huo Ursula von der Leyen na mwenyeji wake Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyyPicha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Pamoja na tangazo hili, Rais Zelensky mwenyewe aliuomba umoja huo kuiwekea vikwazo vikali zaidi Urusi, wakati kukiwa na wasiwasi kwamba vikwazo hivyo vipya vya umoja wa Ulaya havitakidhi matamanio ya Ukraine. Kwa mfano, Ukraine imekuwa ikiomba vikwazo vitakavyolenga sekta ya nyuklia ya Urusi, lakini Hungary, ambako Urusi inatarajia kuweka kinu chake cha nyuklia, tayari imesema kwamba itapigia kura ya turufu ombi kama hilo. 

Maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya wamzuru taifa hilo kuangazia namna watakavyoendelea kuimarisha mahusiano na kufungua njia kwa Kyiv siku moja kujiunga na Umoja wa Ulaya, licha ya mashaka juu yanayoletwa na kashfa za ufisadi. Soma : Zelensky: Urusi yaendeleza mashambulizi mashariki ya Ukraine

Hii ni ziara ya kwanza na ya aina yake kwa ujumbe wa kisiasa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya kutembelea Ukraine, ukiongozwa na von der Leyen mwenyewe pamoja na rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, ambao kwa pamoja wanakutana kesho kwenye mkutano wa kilele na rais Volodymyr Zelensky.