1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakosoa ukandamizaji wa upinzani Uganda

21 Januari 2021

Umoja wa Ulaya umetoa tamko lake kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Uganda kuhusu unyanyasaji dhidi ya wapinzani Uganda wakati wa uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3oEKQ
Frankreich EU-Parlament in Straßburg
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/R. Monaldo

Umoja wa Ulaya umeelezea masikitiko juu ya unyanyasaji na ukandamizwaji uliofanyiwa wanasiasa wa upinzani, wafuasi wao, watendaji wa mashirika ya kiraia pamoja na vyombo vya habari.

Taarifa ya umoja huo imeitaka serikali ya Uganda kutimiza wajibu wake wa kimataifa kwa kuhakikisha kwamba vikosi vya usalama vinajizuia kutumia nguvu kupita kiasi na kuchunguza vitendo vyote vya ukiukaji wa haki za watu

Kadhalika Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa serikali mjini Kampala kuheshimu uhuru wa watu kujieleza na haki ya kuandamana na kukusanyika kwa amani, ikiwemo uhuru wa kutembea kwa wanasiasa na wafuasi wao.

Maafisa wa polisi Uganda wakimkamata mfuasi wa aliyekuwa mgombea urais wa upinzani Bobi Wine. (wilaya ya Luuka, Novemba 18, 2020)
Maafisa wa polisi Uganda wakimkamata mfuasi wa aliyekuwa mgombea urais wa upinzani Bobi Wine. (wilaya ya Luuka, Novemba 18, 2020)Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Hayo yanajiri wakati aliyekuwa mpinzani mkuu wa rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa wiki iliyopita Robert Kyagulanyi akisalia kizuizini tangu alipopiga kura licha ya miito ya kutaka kuachiwa kwake.

Kwenye uchaguzi huo Museveni alitangazwa mshindi lakini upinzani umeyapinga matokeo hayo ukisema uchaguzi ulikumbwa na vitendo vya udanganyifu.