1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Umoja wa Ulaya wajipanga wimbi la wakimbizi wa Afghanistan

31 Agosti 2021

Mawaziri wa sheria na mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanajadiliana juu ya hatua za kuchukuwa kwa wimbi la wakimbizi na wahamiaji linalotazamiwa kutokana na Taliban kuchukuwa madaraka nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/3zjTt
Belgien | Pressekonferenz mit Ylva Johansson und Margaritis Schinas
Picha: John Thys/AP/picture alliance

Mkutano huo ulifanyika siku moja tu baada ya wanajeshi wa mwisho wa Marekani kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kabul usiku wa kuamkia leo, wakihitimisha kile kinachotajwa kuwa vita virefu kabisa kuwahi kupiganwa na Marekani nje ya mipaka yake.

Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Umoja wa Ulaya, Ylva Johansson, aliwaambia waandishi wa habari mjini Brussels mchana wa Jumanne 8Agosti 31) kwamba ilikuwa lazima kwa Ulaya kujitayarisha na chochote kinachoweza kutokea panapohusika suala la wakimbizi wa Afghanistan.

Umoja huo wenye mataifa 27 wanachama ulikuwa unasaka namna ya kuzuwia kurejea kwa mzozo wa wakimbizi wa mwaka 2015 ambao ulichangiwa sana na kushamiri kwa vita nchini Syria. 

"Kila mmoja anataka kukwepa hali kama ile ya 2015, na tunaweza kuiepuka, tumejitayarisha zaidi safari hii, na tunaweza kuafikiana kuanza sasa kufanya matayarisho. Hatupaswi kungojea hadi watu wapo mipakani. Ila ili kuweza kufanya hayo, lazima tushirikiane, jambo ambalo nadhani mataifa wanachama wanakubaliana kulifanya," alisema Bi Johansson.

Kumbukumbu za mzozo wa 2015

Polen | Grenzzäune zwischen Polen und Belarus
Wanajeshi wa Poland wakilinda mpaka wenye seng'enge ya waya kuzuwia wakimbizi kuingia.Picha: Dominika Zarzycka/NurPhoto/picture alliance

Kuwasili kwa zaidi ya wakimbizi milioni moja mwaka huo barani Ulaya kulizusha malumbano makali kati ya wanachama wa Umoja wa Ulaya juu ya namna ya kulidhibiti wimbi hilo. Na kwa kuporomoka kwa serikali iliyoungwa mkono na mataifa ya Magharibi na kuingia madarakani kwa kundi la Taliban nchini Afghanistan, kunaweza kupelekea hali kama hiyo, kwa mujibu wa Kamishna huyo wa Mambo ya Ndani wa Ulaya.

Hata hivyo, huenda mtazamo wa Umoja wa Ulaya wa kuwaweka wakimbizi kutoka Afghanistan katika mataifa yaliyo karibu na nchi hiyo usiyapendeze mashirika ya haki za binaadamu.

Katika barua yake kwa Johansson, shirika la Amnesty International liliutaka Umoja wa Ulaya usitumie dhana ya kulinda mipaka yake kama kisingizio cha kukwepa  wajibu wake wa kimataifa wa kuwalinda watu wanaoomba hifadhi. 

"Umoja wa Ulaya na Mataifa Wanachama lazima wawape Waafghani fursa ya kuingia kwenye nchi zao na kuwawekea mfumo wa haki na wenye ufanisi wa kuwapa hifadhi na pia kujenga mazingira yanayokubalika ya kuwapokea", ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosisitiza kwamba "wanawake na wasichana wapewe kipaumbele."

Hadi inamaliza duru yake ya mwisho ya kuwaondowa wanajeshi wake usiku wa kuamkia tarehe 31 Agosti 2021, Marekani ilisema kuwa ilishawahamisha raia 120,000 wa Kimarekani, wageni na Waafghani.

Kwa mujibu wa makisio ya Umoja wa Ulaya, takribani Waafghani 570,000 waliomba hifadhi barani humu tangu mwaka 2015, lakini idadi ilipanda mara tatu zaidi tangu mwezi Februari mwaka huu, ilipobainika wazi kuwa majeshi ya kigeni yangeliondoka.