1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waidhinisha tume ya kijeshi Mediterania

19 Mei 2015

Nchi za Umoja wa Ulaya zimeidhinisha tume ya kijeshi katika bahari ya Mediterania kuanzia mwezi ujao kupambana na wafanyabiashara ya kuuza binaadamu waliosababisha wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Libya kuingia Ulaya.

https://p.dw.com/p/1FRk0
Mittelmeer Küstenwache Italien Flüchtlingsboot Flüchtlinge Rettung
Picha: Picture-alliance/epa/Italian Coast Guard

Harakati hiyo iliyoungwa mkono na mawaziri wa mambo ya nchi za kigeni na wa ulinzi mjini Brussels utazijumuisha meli za kivita za nchi za Ulaya na ndege za kukusanya taarifa za kijasusi na baadaye kuzivamia boti kuwakabili wafanyabiashara ya kusafirisha watu.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini alisema uamuzi huo uliopitishwa katika mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni na wa ulinzi utatatiza biashara ya walanguzi na mitandao ya wasafirishaji binaadamu katika bahari ya Mediterania.

"Huu ni mwanzo tu. Uamuzi wa kuanzisha operesheni unamaanisha sasa mchakato wa kupanga utaratibu wenyewe umeanza. Ningependa operesheni hii ianze haraka iwezekanavyo ikiwezekana mwezi ujao kama tunataka kuyazuia mashirika ya wafanyabiashara ya kuuza na kusafirisha binaadamu."

Serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa mjini Tobruk inaupinga mpango huo na ilisema Umoja wa Ulaya sharti ushauriane nayo kwanza. Lakini Mogherini alithibitisha umoja huo unawasiliana na serikali zote mbili za Libya na alisema mchakato wa kuratibu tume hiyo NAVFOR MED utaanza mara moja. Tume hiyo itakakuwa na makao yake makuu mjini Roma, Italia na kuongozwa na Mkuu wa jeshi la wanamaji la Italia.

EU Mogherini beim EU-Außen- und Verteidigungsministertreffen
Mogherini (katikati) akiwa katika mkutano wa BrusselsPicha: Reuters/F. Lenoir

Tume hiyo ambayo itakuwa na awamu tatu kuanzia kukusanya taarifa za kijasusi, kuzivamia na kuingia boti za walanguzi na hatimaye kuziharibu, huenda ikazinduliwa rasmi mwezi ujao baada ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya unataka hatimaye kuwakamata walanguzi na kuziharibu boti zao nje ya pwani ya Libya kusaidia kudhibiti idadi inayoongezeka ya wakimbizi wanaokimbia vita na umaskini Afrika Kaskazini, lakini nchi nyingi za umoja huo zinataka kwanza idhini ya Umoja wa Mataifa kuchukua hatua hiyo.

Idhini ya Umoja wa Mataifa yahitajika

Bila idhini ya Umoja wa Mataifa tume ya kijeshi ya Umoja wa Ulaya haitakuwa na mamlaka ya kuingilia kati katika eneo la bahari ya Libya na hata nchi kavu kuvikamata vyombo vya baharini vinavyotumiwa kusafirishia watu. Lakini wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wanaweza kuanza kutumia meli na helikopta baharini kukusanya taarifa za kijasusi kuhusu walanguzi wa watu.

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier alisema wazo la kuunda tume hiyo limekubaliwa bila kauli za kulipinga na majadiliano yanaendelea. Alisema hatua zitakazofuata zitaanzishwa wakati misingi ya kisheria itakapofafanuliwa, jambo ambalo pia lilijadiliwa bila mabishano yoyote.

"Kama tunataka kuzisimamisha meli baharini, kama tunataka kuingia katika meli, kama tunataka kufanya shughuli zetu katika eneo la bahari ambalo ni himaya ya Libya, basi tunahitaji azimio kutoka kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo hadi leo hatujui kama litakuja kuiidhinishwa."

Deutschland Bundestag Frank-Walter Steinmeier
Frank Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/L. Schulze

Austria ilisema itaipinga tume hiyo kama haitakuwa na idhini ya Umoja wa Mataifa.

Jumuiya ya NATO yataka kusaidia

Wakati huo huo katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, aliyehudhuria pia mkutano wa Brussels, alisema jumuiya hiyo inayoongozwa na Marekani iko tayari kusaidia lakini Umoja wa Ulaya haujaomba msaada. Pia alionya kwamba magaidi kutoka makundi yenye misimamo mikali yumkini wanavuka bahari wakijificha miongoni mwa wakimbizi.

Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania tayari ziliahidi kupeleka meli za kivita kwa tume hiyo ya pamoja ya kijeshi ya Umoja wa Ulaya ambayo si ya kawaida kwa kanda iliyoundwa kuimarisha amani baada ya kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip Hammond alisema mawaziri wanahitaji kutayarisha mpango kamili. Alisema ushirikiano na Libya ni muhimu.

Mwandishi:Josephat Charo/DPAE/AFPE/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman