Umoja wa Ulaya, Uingereza zarejea kwenye meza ya mazungumzo
19 Oktoba 2020Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Maros Sefcovic, aliwaambia waandishi wa habari mjini Brussels kwamba mkutano wake na waziri mwenye dhamana ya Brexit kwenye serikali ya Uingereza, Michael Gove, asubuhi ya Jumatatu (Oktoba 19) ulikuwa na mafanikio makubwa.
Mkutano huo ulifanyika baada ya mazungumzo ya kusaka makubaliano ya kibiashara kati ya pande hizo mbili kuonekana kuvunjika wiki iliyopita, huku kila upande ukiutaka mwengine kubadili sera zake.
"Tumeangazia zaidi juu ya utekelezwaji muafaka na wa wakati wa makubaliano ya kujiondowa. Tumejikita kwenye haki za raia, na nadhani tunaendelea vyema, na nina hakika kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka huu, tutakuwa tumeshatuliza akili za Uingereza na Ulaya na mpango wa utekelezaji utakuwa tayari," alisema Sefcovic.
Hadi Jumapili asubuhi, Gove, alikuwa akiamini kwamba nafasi ya pande hizo mbili kufikia muafaka ilikuwa finyu sana. Alikiambia kituo cha televisheni cha BBC kwamba hata kama walikuwa wanatarajia Umoja wa Ulaya kubadili msimamo wake, "ilikuwa haki kuwasiliana pale ambapo sote tuko tayari."
Chanzo cha mkwamo wa sasa
Hasa mkwamo ulizuka pale Uingereza ilipotangaza sheria mpya inayoiruhusu serikali kufuta sehemu za makubaliano ya nchi hiyo kujitowa Umoja wa Ulaya zinazohusiana na biashara na Ireland ya Kaskazini, sehemu pekee ya Muungano wa Ufalme wa Uingereza inayopakana na Umoja wa Ulaya.
Rasimu ya sheria hiyo ilichochea mgogoro wa kutoaminiana baina ya pande hizo mbili, ambazo zimekuwa zikijaribu kupata makubaliano mapya ya kibiashara tangu Uingereza ijiondowe Umoja wa Ulaya mnamo tarehe 31 Januari.
Umoja huo ulisema ungelipendelea kuendelea na mazungumzo lakini serikali ya Uingereza ikasema mazungumzo kati yao yalikuwa yamekwisha, vyenginevyo kuwe na mabadiliko ya kimsingi kwenye msimamo wa Umoja wa Ulaya.
Mbali ya Sefcovic na Gove, wajumbe wengine waliotazamiwa kuwa na mazungumzo ya Jumatatu walikuwa mkuu wa timu ya upatanishi ya Umoja wa Ulaya, Michel Bernier, na mwenzake wa Uingereza, David Frost.
Ikiwa hakutakuwa na makubaliano, biashara za pande zote mbili zitakabiliwa na vikwazo vya ushuru na vyengine kadhaa kuanzia tarehe 1 Januari.