1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Umoja wa Ulaya: Tutaisaidia Ukraine bila kuchoka

10 Februari 2023

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekamilisha mkutano wa kilele mjini Brussels alfajiri ya Ijumaa kwa ahadi ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine "bila kuchoka" ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuipatia nchi hiyo ndege za kivita.

https://p.dw.com/p/4NJXh
Belgien Brüssel | EU-Gipfel
Picha: John Thys/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ulimalizika baada ya saa 16 za majadiliano makali juu ya suala la Ukraine pamoja na ajenda nyingine muhimu ya kudhibiti idadi ya wahamiaji kwenye mataifa ya Ulaya.

Kuhusu Ukraine, viongozi wa kanda hiyo wametoka na kauli moja tu,  ya kuendelea kulisaidia taifa hilo lililo vitani bila kuchoka na kuahidi kufanya inavyowezekana kuiwezesha kuzishinda hujuma za Urusi.

Mkutano huo ulitiwa ari zaidi na uwepo wa rais Volodymyr Zelenskyy ambaye alifanya ziara mjini Brussels kuzungumzia moja kwa moja mahitaji ya Ukraine mbele ya viongozi wa Ulaya.

Ingawa wakati mkutano huo unamalizika rais Zelensky alikuwa tayari ameondoka ukumbini, viongozi wa mataifa Ulaya wamesema katu hawataitupa mkono Ukraine hadi ishinde vita dhidi ya Urusi.

Ombi la Ukraine kupewa ndege za kivita linaweza kutimizwa na Ulaya 

Belgien Brüssel | EU-Gipfel | Emmanuel Macron
Rais Emmanuel Macron wa UfaransaPicha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema yeye binafsi haondoi uwezekano wa kuipatia Ukraine ndege za kivita kama ilivyoombwa na rais Zelensky.

Msimamo huo umeelezwa pia na waziri mkuu wa Finland Sanna Marin alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya iwapo yuko tayari kuipatia Ukraine ndege za kivita.

"Sitaki kuondoka uwezekano wa chochote kwenye hatua hii. Nadhani ni muhimu kutuma ujumbe bayana na ishara kwa Ukraine na raia wake kwamba tumedhamiria kutoa msaada kwa njia yoyote, na ikibidi kwa kipindi chote (cha mzozo) na ni sharti tujadili kuhusu silaha nzito" amesema Bibi Marin.

Suala la Ukraine kupatiwa ndege za kivita ndiyo ilikuwa ajenda ya wazi ya rais Zelensky alipofanya ziara ya siku tatu barani Ulaya. Aliliweka mezani alipokuwa mjini London nchini Uingereza Jumatano asubuhi, akalitaja tena alipokutana na rais Macron na kansela Olaf Scholz wa Ujerumani mjini Paris jioni ya Jumatano na kulizungumza kwa mara nyingine alipozuru makao makuu ya Umoja wa Ulaya jana Alhamisi.

Zelensky asema wengi ya viongozi wanaweza kuidhinisha msaada wa ndege 

EU Ukraine Selenskyj in Brüssel
Rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky (katikati) akiwa na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Yeye mwenyewe rais Zelensky amesema viongozi kadhaa wa Ulaya aliozungumza nao wameonesha utayari wa kuipatia nchi yake ndege za kivita.

Akiwa mjini Brussels Zelenskyy alimuomba moja kwa moja waziri mkuu wa Slovakia Eduard Heger ndege za kivita za enzi ya Muungano wa Kisovieti aina ya MiG chapa 29 ombi ambalo Heger alijibu atalifanyia kazi.

Mbali ya suala la ndege ambalo baadhi ya viongozi wamesema ni pendekezo litakalochukua muda mrefu kuafikiwa, mkutano wa mjini Brussels umekubaliana kutizama uwezekano wa kuongeza uzalishaji wa silaha kwa ajili ya Ukraine kuanzia mwezi ujao kama msaada wa haraka.Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesema kanda hiyo itafaa ifanye kazi na sekta ya viwanda kuhakikisha kasi ya kutengeneza risasi na mabomu inaongezwa kutimiza mahitaji yaliyopo Ukraine.Hata hivyo suala ambalo kwa mara nyingine halikupewa umuhimu mkubwa ni shinikizo la Ukraine la kutaka kujiunga haraka na Umoja wa Ulaya. Yumkini suala hilo bado litasubiri kwa sasa.