1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU, NATO kuipa msaada Uturuki

Sekione Kitojo
10 Machi 2020

Rais wa  Uturuki ameitaka jumuiya  ya  NATO kuonesha mshikamano  zaidi  na  Uturuki. Kwa  upande  wa  Umoja  wa  Ulaya kuna  hali ya  kupishana kimtazamo, lakini pia imeahidi kuipa Uturuki msaada.

https://p.dw.com/p/3Z85W
Belgien Gespräch von der Leyens mit Erdogan ohne erkennbares Ergebnis
Picha: picture-alliance/dpa/D. Pignatelli

Tumo  katika mkanganyiko, amesema  rais  wa halmashauri  ya  Umoja  bwa Ulaya  Ursula von der Leyen baada ya  kukutana  na  Erdogan  mjini Brussels jana, lakini  makubaliano kuhusu  wakimbizi yataendelea. 

Brüssel | Pressekonferenz Ursula von der Leyen und Charles Michel nach Treffen mit Erdogan
Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen (kushoto) na rais wa baraza la Ulaya Charles Michel (kulia)Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Hali  katika  jimbo  la  Idlib  ni kitisho  kwa  Ulaya  yote, amesema  rais  wa  Uturuki  Recep Tayyip Erdogan  alipokutana  na katibu  mkuu  wa  NATO  Jens Stoltenberg. na  hakuna  mtu anaweza  kuangalia  kwa  njia nyingine  mzozo  wa  kiutu katika  eneo  hilo. Uturuki imefanya  vya  kutosha  kuliko nchi  nyingine  mwanachama  wa NATO, ndio  sababu  nchi  hiyo inatarajia  mshikamano.

Recep tayyip Erdogan  akiwa  mwenye kujiamini  alikutana  na wawakilishi  wa  NATO , ambao walizungumzia  kuhusu  kufanya tafakuri  juu  ya  kutoa  msaada kwa  Uturuki. Wakati  huo huo lakini  wawakilishi  hao  wa  NATO waliitaka  Uturuki  kutafuta suluhisho  la  muda  mrefu katika  Syria , na  kumkumbusha rais  Erdogan , kwamba  kwa hatua  yake  ya  kununua  mfumo wa  kukinga  makombora  kutoka Urusi  amejikuta  bila  marafiki. Akizungumza  katika  mkutano  na waandishi  habari  pamoja  na rais  wa  Uturuki, Recep Erdogan, katibu mkuu  wa  NATO  Jens Stoltenberg  alisema:

Rauchbomben und Tränengas an griechisch-türkischer Grenze
Wakimbizi wakipigwa mabomu ya kutoa machozi na polisi wa Ugiriki katika mpaka kati ya Uturuki na UgirikiPicha: Reuters/H. Aldemir

"Hakuna  mshirika  wetu  mwingine yeyote  aliyeathirika zaidi na mashambulizi  ya  kigaidi, na hakuna  mshirika anayewahifadhi wakimbizi wengi zaidi. NATO itaendelea  kuiunga mkono Uturuki kwa  hatua  kadhaa tofauti."

Kwa upande  wa  Umoja  wa  Ulaya unabaki  katika  dhamira yake katika  mkataba  wa  wakimbizi na  makubaliano  hayo yataendelea  kuwa hai, rais  wa halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya Ursula von der Leyen  alisema jana  jioni  baada  ya  kukutana na  rais  wa  Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini  Brussels. Mazungumzo  hayo  yalifanyika baada  ya  mvutano wa  siku kadhaa  kati  ya  Umoja  wa Ulaya  na  Uturuki  kuhusiana  na suala  la  wahamiaji  katika mpaka  kati  ya  Uturuki  na Ugiriki. Rais wa  halmashauri ya Umoja  wa  Ulaya  Ursula von der Leyen akizungumza  katika mkutano  na  waandishi habari amesisitiza kuhusu msaada  kwa Uturuki.

"Wahamiaji wanahitaji msaada, Ugiriki inahitaji  msaada, lakini pia Uturuki inahitaji  kuungwa mkono , na  hii  inahusu kupatikana  njia  kuelekea mbele pamoja  na  Uturuki. Bila shaka  tuna tofauti  zetu  lakini tumezungumza  wazi  juu ya  haya na  yalikuwa mazungumzo  mazuri, yalikuwa majadiliano  mazuri  na yalikuwa  yenye  manufaa."

Belgien | Pressekonferenz Ursula von der Leyen und Charles Michel nach Treffen mit Erdogan
Rais wa baraza la Ulaya Charles MichelPicha: Reuters/F. Lenoir

Von der Leyen  amesema  kuwa tathmini  itafanyika  kuhusu sehemu  gani  ya  makubaliano haijatekelezwa  na  kwa  nini. Pia  akizungumza  baada  ya mkutano  huo , rais  wa  baraza la  Ulaya  Charles Michel  amesema mkuu  wa  sera  za  mambo  ya kigeni  wa  Umoja  huo  na  waziri wa  mambo  ya  kigeni  wa Uturuki wanapaswa  kufanyakazi kwa  pamoja  na  timu  ya wataalamu  na  kutoa  ufafanuzi wa  tofauti  za  mawazo zilizopo katika  utekelezaji wa makubaliano katika  muda  wa siku  chache  zijazo.