1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kujadili kuhusu mkutano wa kilele na Putin

24 Juni 2021

Umoja wa Ulaya utajadili Alhamis kuhusu uwezekano wa kufanya mkutano wa kilele na Rais Vladmir Putin wa urusi kama sehemu ya mkakati mpya wa kushughulikia uhusiano na Moscow ambao umoja huo unasema umo katika mdororo.

https://p.dw.com/p/3vUlF
Belgien EU Wladimir Putin in Brüssel
Picha: Getty Images/AFP/G. Gobet

Mabalozi kutoka Ufaransa na Ujerumani walipendekeza jana kwamba kufanya mkutano wa kilele na Putin ilikuwa njia inayoweza kurekebisha mahusiano kati ya washirika hao wa karibu wa kibiashara, kama alivyofanya Rais Joe Biden wa Marekani  na Putin mjini Geneva.

Wakiwa pande kinzani katika mikwamo nchini Ukraine na Belarus, na katika mikwaruzano kuhusu haki za binadamu, Umoja wa Ulaya na Urusi zinashutumiana kwa kuingilia kati uchaguzi, kampeni za upotoshaji na kutishia usalama na utulivu kuanzia mataifa ya Baltic hadi Bahari nyeusi.

Urusi iko katika mzozo na mataifa kadhaa ya Magharibi

Akizungumza jana bungeni, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema Umoja wa Ulaya unapaswa kutafuta mazungumzo ya moja kwa moja na rais Vladmir Putin hata wakati ukisimama pamoja dhidi ya uchokozi kutoka Urusi, na kuongeza kuwa haitoshi tu kwa rais wa Marekani kuzungumza na rais wa Urusi.

Bundestag Angela Merkel Befragung Bundesregierung
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

"Matukio ya miezi ya karibuni, siyo tu nchini Ujerumani, yameonesha wazi kwamba haitoshi kwetu kujibu katika njia isiyoratibiwa dhidi ya uchokozi wa Urusi. Badala yake tunapaswa kuunda mfumo kwa kujibu uchokozi huo kwa pamoja. Hii ndiyo njia pekee kwetu kujifunza namna ya kukabiliana na mashambulizi mchanganyiko ya Urusi," alisema Merkel.

Urusi iko katika mzozo na mataifa kadhaa ya Magharibi baada ya kurundika wanajeshi wake kwenye mipaka ya Ukraine na mkururo wa kashfa kadhaa za ujasusi zilizopelekea kufukuziana wanadiplomasia.

Katika kisa cha karibuni cha mzozo, Ujerumani ilimkamata mwanasayansi wa Urusi anayefanya kazi katika chuo kikuu cha Ujerumani, ikimshutumu kwa kuifanyia upelelezi Moscow.

Ukraine imekosoa kufanyika mkutano wa kilele na Putin

Kuendelea kushikiliwa kwa mkosoaji wa Kremlin, Alexei Navalny, ambaye alipatiwa matibabu mjini Berlin baada ya tukio la kupewa sumu lililokaribia kukatisha maisha yake, pia kumesababisha hasira katika Umoja wa Ulaya.

Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, amekosoa mapendekezo hayo ya kuanzisha tena mikutano ya kilele na Urusi, akisema baada ya kukutana na mkuu wa sera ya kigeni ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, kwamba kuchukua hatua kama hiyo bila kuona maendeleo yoyote kutoka upande wa Urusi utakuwa ukengeukaji hatari wa sera ya vikwazo ya Umoja wa Ulaya.

Ukraine Präsident Wolodymyr Selenskyj in Kiew
Rais wa Ukraine Volodomyr ZelenskyPicha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Mkutano wa leo wa kilele wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya ndiyo wa mwisho kwa Kansela Angela Merkel kabla ya uchaguzi utakaoamua mrithi wake mwezi Septemba mwaka huu. Merkel alichukuliwa kama kiongozi miongoni mwa mataifa wanachama wa kanda hiyo katika kushughulika na Putin, wakati uhusiano baina ya Ulaya na Urusi ukiharibika katika muda wa miaka saba iliyopita.