1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

UN yatafuta dola bilioni 4.44 kuisaidia Afghanistan

31 Machi 2022

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ikiungwa mkono na Uingereza,Ujerumani na Qatar imeanzisha juhudi kubwa za kuchangisha kuisadia Afghanistan

https://p.dw.com/p/49H0C
Afghanistan | Bäckerei in Kabul spendet Brot
Picha: Ali Khara/REUTERS

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ikiungwa mkono na Uingereza,Ujerumani na Qatar imeanzisha juhudi kubwa za kuchangisha fedha kwa ajili ya kuisadia Afghanistan,nchi inayotawaliwa na kundi la Wanamgambo la Taliban.

Wakati ulimwengu ukiwa umejielekeza  kwa kiaasi kikubwa katika vita vya Urusi nchini Ukraine Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada imeamua kuanzisha juhudi kubwa  zenye lengo la kuchangisha dola bilioni 4.44 kwa ajili ya kuisadia Afghanistan.

Martin Griffiths
Picha: UN/Mark Garten

Martin Griffiths ambaye anaongoza ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu  akizungumza kabla ya kuanzishwa rasmi juhudi za kuchangisha hii leo ameutanabahisha ulimwengu kwamba Ukraine ni muhimu sana lakini Afghanistan inauhitaji ulimwengu kuionesha umejitolea na unaiunga mkono. Griffiths ametowa rai kwa dunia kuisaidia nchi hiyo iliyotumbukia kwenye umasikini.

    " Tunawaomba wafadhili leo hii kuchangisha  katika juhudi hizi kubwa za msaada wa kibindamu ambao haujawahi kufanywa kwa nchi moja. Tunaomba mchango wa dola bilioni 4.44  kuwasaidia wananchi wa Afghanistan katika kipindi kigumu walichonacho cha uhitaji katika mwaka huu. Nawatolea mwito wafadhili kuongeza juhudi na kutoa ahadi ya mchango mkubwa kwa kile  ninachoamini ni moja ya mgogoro mkubwa wa kibinadamu  duniani.''

Tayari ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inaungwa mkono na Uingereza,Ujerumani na Qatar katika juhudi hizo za kuichangia Afghanistan ikiwa ni chini ya mwaka mmoja baada ya kundi la wapiganaji wa Taliban kuiondowa madarakani serikali iliyokuwa ikiungwa mkono kimataifa. Hivi sasa nchi hiyo imezama kwenye mgogoro mkubwa wa kibinadamu na kiuchumi ambapo kiasi watu milioni 23 wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula,kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Griffiths jana Jumatano aliwaambia waandishi habari, uchumi wa taifa hilo ni dhaifu sana kusimamia maisha ya kila siku ya wananchi wake,wanawake na watoto na kwahivyo nchi wafadhili hazina budi kutowa mchango mkubwa kuwasaidia waafghanistan.

Symbolbild I United Nations Emblem
Picha: John Angelillo/UPI/newscom/picture alliance

Fedha zinazohitajika ni nyingi mara tatu ya zile Umoja huo wa mataifa ulizoomba kwa ajili ya taifa hilo mwaka jana . Kwa upande mwingine kiongozi wa  China Xi Jinping hii leo ametowa tamko zito la kuiunga mkono Afghanistan akiwa katika mkutano wa kikanda,bila ya kugusia chochote kuhusu visa vya ukiukaji haki za binadamu vinavyofanywa na viongozi wa Taliban wanaotawala nchi hiyo. Xi ametoa tangazo hilo mbele ya mkusanyiko uilohudhuriwa na wajumbe kutoka Afghanistan,China Urusi,Pakistan,Iran,Tajikistan,Turkmenistan na Uzbekistan uliofanyika huko huko China.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW