1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu vurugu Myanmar

17 Februari 2021

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayefuatilia hali ya haki za binadamu Myanmar, Thomas Andrews, ameonya kuhusu uwezekano wa kuzuka vurugu wakati ambapo wanaandamanaji wanakusanyika tena leo kupinga mapinduzi ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/3pSu9
Myanmar Proteste nach Militärputsch
Picha: AP Photo/dpa/picture alliance

Andrews amesema amepokea taarifa za wanajeshi kupelekwa kwenye mji mkubwa zaidi wa Yangon, kutoka kwenye miji mingine.

Katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake mjini Geneva, mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema katika kipindi cha nyuma wanajeshi hao walifanya mauaji, watu kutoweka na watu wengi kuwekwa kizuizini.

Maandamano zaidi yanatarajiwa kufanyika Jumatano nchi nzima, licha ya uwezekano wa kuzuka makabiliano ya jeshi na polisi.

Siku ya Jumatatu vikosi vya usalama viliwaelekezea bunduki umati wa waandamanaji 1,000 kwenye mji wa Mandalay na kuwashambulia kwa manati na fimbo.