1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya athari za ujoto kwa nchi tajiri

Siraj Kalyango11 Desemba 2007

Japan yaupigia upatu mkataba wa Kyoto

https://p.dw.com/p/Ca6K
Mohammad, 32, akiloa samaki kutoka maji ya kidimbwi cha umma ambayo yamechafuliwa mno katika eneo la Bali Indonesia.Kwa mujibu wa wanamazingira,kisiwa cha Bali kinakabiliwa na mgogoro wa kimazingira baada ya mito kukizunguka kuchafuliwa na uchafu wa viwanda vya karibu.Picha: AP

Mkutano wa hali ya hewa ukiendelea Bali- Indonesia,ripoti maalum kuhusu hali ya hewa imeonya kuwa athari za kubadilika kwa hali ya hewa kutaweza kuwa ghali mno na utazilazimisha nchi zilizoendelea kuchangia dola billioni 86 kila mwaka ifikapo mwaka wa 2015 ili kuzisaidia nchi maskani.

Ripoti ya maendeleo ya binadamu imeonya kutokea kile ilichokiita mwelekeo wa kibaguzi kuhusu kubadilika kwa hali ya hewa.Alieandika ripoti hiyo ya Umoja wa Mtaifa, Kevin Watkins,amesema katika mkutano wa Bali kuwa nchi maskaini duniani hazihusiki kamwe na ujoto duniani.Ameongeza kuwa nchi zilizoendelea, kwa kuwa ndizo zimesababisha mgogoro huu, ni lazima ziwajibike, mkiwemo kuwalinda waathiriwa.

Ripoti hiyo imeonya dhidi ya 'mwelekeo wa kibaguzi' ikiwa nchi tajiri zitawekeza katika 'teknolojia safi 'na nchi maskani kuziacha 'kuzama'.

Mwito kama huo umetolewa na mkuu wa tume ya kiserikali kuhusu kubadilika kwa hali ya hewa IPCC- Rachendra Pajauri mjini Oslo wakati wa kutoa tuzo la mazingira ambapo makamu rais wa zamani wa Marekani-Al Gore alitunukiwa tuzo la Nobel la mwaka huu wa 2007,

‚…swali ni ikiwa washiriki wa mkutano wa Bali wataunga mkono juhudi hii. Na je! Wale wote wanaohusika na kutoa maamuzi ya kubadilika kwa hali ya hewa katika ngazi ya kimataifa,watasikia kauli ya wanasayansi ambayo iko wazi?Ikiwa watafanya hivyo katika mkutano wa Bali na kwingineko hapo baadae,wenzangu wote katika kamati ya mataifa kuhusu kubadilika kwa hali ya hewa ya IPCC- na maelefu wengine wanaofanya kazi kwa ajili ya sayansi,watahisi wamepewa heshima kubwa –hasa wakati huu nikipokea tuzo kwa ajili’ asema Pajauri.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ni kama inazionya nchi zenye viwanda vingi hasa Marekani kuchukua hatua ya kuona kuwa upunguzaji wa utoaji wa gesi chafu unaimarishwa.Marekani baado inakataa kuheshimu mkataba wa Kyoto ambao hivi karibuni utafikia kikomo.Kwa upande mwingine waziri wa mazingira wa Japan ameufananisha mkataba wa Kyoto kama mtoto mwenye uchu lakini mgumu. Waziri huyo ameomba kuwe na uelewano ili kuimarisha mwangaza wa mkataba huo.Waziri Ichiro Kamoshita alikuwa anaadhimisha miaka 10 ya mkataba huo katika mji wa Bali ambapo nchi 190 na ushei zinajaribu kutafuta njia za kukabiliana na ujoto baada ya ule wa Kyoto kufikia kikomo mwaka wa 2012.

Mkataba huo ulipewa jina hilo kutokana na kuwa ndiko huko majadiliano kuuhusu yalifanyika mwongo mmoja uliopita. Hii ilikuwa ndio mwanzo wa kujaribu kupunguza utoaji wa gesi chafu zinazolaumiwa kwa kuharibu mazingira kama vile gesi ya kaboni.

Mkataba huo wa kihistoria kidogo usambaratike mwaka wa 2001 wakati Marekani , namba moja katika uchafuzi wa mazingira, kuugomea.Aidha utekelezwaji wake pia ulipata wasiwasi pale nchi nyingi zikitaka fidia katika kuangamia kwa misitu yake.Baada ya matatizo ya hapa na pale mkataba huo ulianza kutumika mwaka wa 2005. Japan imeupigia sana upatu, ingwa ulipingwa na mshirika wake wa karibu- Marekani.

Hata nayo Japan, ambayo uchumi wake unazidi kuimarika baada ya kipindi kigumu cha mwaka wa 1990, baado haijafikia kiwango ilichopewa na mkataba huo.Japan ilibidi kupunguza hadi asili mia 6 ya utoaji wa gesi chafu, lakini hadi sasa inatoa asilia mia nane.Aidha wana mazingira pia wameilaumu Japan kwa kupinga shabaha kali ya kiwango cha mwaka 2012.