1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wajitolea kupatanisha Libya

4 Machi 2022

Umoja wa Mataifa umejitolea kupatanisha mzozo uliozuka Libya juu ya mfumo wa kufuatwa baada ya kuahirishwa uchaguzi na kuundwa kwa serikali inayopingwa na upande mmoja, huku ukionya dhidi ya kuzorota kwa hali ya usalama.

https://p.dw.com/p/481Rl
Schweiz Libysches Dialogforum in Genf
Picha: UNITED NATIONS/AFP

Afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa, Stephanie Williams, alitowa pendekezo hilo siku moja tu baada ya bunge la mashariki mwa Libya kumuapisha waziri mkuu mpya, likipingana na uamuzi wa waziri mkuu wa kipindi cha mpito, Abdulhamid Dbeibah, aliyekataa kujiuzulu. 

Mshauri huyo maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, alionya siku ya Ijumaa (Machi 4) kupitia ukurasa wa Twitter kwamba "suluhu la mzozo wa Libya halipatikani kwa kuunda tawala na mabaraza tafauti ya uongozi."

Alisema alishawaandikia viongozi wa pande zote mbili - wale wa Baraza la Wawakilishi lilipo mashariki na Baraza Kuu la Nchi lililopo Tripoli - akiwataka "kuteuwa wajumbe sita kila upande na kuunda kamati ya pamoja itakayojikita kwenye kusaka maridhiano kwa misingi ya kikatiba."

Pendekezo la Stephanie Williams lilikuja baada ya chaguzi za bunge na rais zilizokuwa zifanyike Disemba 24 kama sehemu ya mchakato wa amani uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa kutelekezwa kukiwa na mtafaruku mkubwa juu ya uhalali wake kisheria na kikatiba na pia ugombeaji wa nafasi kadhaa za juu. 

Mzozo mpya wa utawala

Die zwei libyschen Führer Abdul Hamid Dbeibah und Fathi Bashagha
Waziri mkuu mpya wa Libya aliyeapishwa na bunge la mashariki, Fathi Bashagha, na waziri mkuu wa sasa ambaye amekataa kujiuzulu, Abdulhamid Dbeibah.Picha: picture-alliance

Usitishwaji huo usio kikomo wa uchaguzi uliyapoteza matumaini yaliyokuwepo ya kufunuwa ukurasa mpya baada ya machafuko ya muongo mzima yaliyoanza kwa ghasia za mwaka 2011 zilizomng'owa kiongozi wa muda mrefu, Muammar Gaddafi.

Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika lilikuwa na serikali mbili hasimu kutoka mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa 2021, pale utawala wa Dbeibah uliporidhiwa na makundi makuu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano mwishoni mwa mwaka 2020.

Jana, Alkhamis, licha ya juhudi za miezi kadhaa za Umoja wa Mataifa zilizolenga kuziunganisha taasisi zake, Libya ilijikuta tena kwenye mkwamo kwa kuwa na mawaziri wakuu wawili - Dbeibah mwenye makao makuu yake mjini Tripoli, ambaye alikataa kukabidhi madaraka bila ya kupatikana serikali iliyochaguliwa, na waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Fathi Bashagha, ambaye anaungwa mkono na bunge la upande wa mashariki.

Kwenye hotuba yake baada ya kuapishwa, Baghasha alimtuhumu Dbeibah na washirika wake kwa kufunga anga la nchi na kuwatia nguvuni mawaziri watatu kuwazuia kufika bungeni hapo kuapishwa. 

Stephanie Williams amependekeza mkutano baina ya pande hizo mbili ufanyike tarehe 15 mwezi huu wa Machi, ingawa hadi sasa hakujawa na majibu yoyote kutoka pande husika.