1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wahofia mzozo wa Sudan kuongeza wakimbizi

28 Juni 2023

Umoja wa Mataifa unasema machafuko yanayoendelea nchini Sudan yana uwezekano mkubwa wa kusababisha watu wengine milioni moja kuikimbia nchi hiyo, huku mkuu wa majeshi akitowa wito kwa vijana kujiunga na vita.

https://p.dw.com/p/4T9VO
Sudan Kämpfe
Picha: Stringer/IMAGESLIVE via ZUMA Press Wire/picture alliance

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa jioni ya Jumanne (Juni 26) ilisema licha ya ghasia hizo kuelekezwa kwa kiasi kikubwa kwenye mji mkuu, Khartoum, ambako jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah Burhan na wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo wanawania udhibiti, mauaji makubwa yanashuhudiwa pia jimbo la magharibi la Darfur, ambako wanamgambo wa Dagalo na washirika wao wa Kiarabu wanawaandama raia wa makabila mengine yasiyo ya Kiarabu.

Soma zaidi: Sudan yageuka uwanja wa mapigano kwa wapiganaji wa kigeni
Sudan: Makubaliano ya usitishwaji mapigano kufikia tamati

Mwishoni mwa wiki, Sultan Dar Masalit, kiongozi wa jamii ya Masalit ambao ni Wasudan weusi, aliwatuhumu wanamgambo hao wa Kiarabu  na RSF kwa "kufanya mauaji ya maangamizi dhidi ya Waafrika."

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, watu 5,000 wameuawa ndani ya kipindi cha miezi miwili iliyopita, wengi wao kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Genena.

Sudan Flüchtlinge auf einem Lastwagen
Watu wakihama na vitu vyao kukimbia mapigano mjini Khartoum.Picha: AFP

Hata hivyo, idadi rasmi iliyotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu vifo vilivyosababishwa na mzoo huo kote nchini Sudan ni vya watu 3,000, huku ukiwageuza wengine milioni 2.5 kuwa wakimbizi wa ndani na nje, wengi wa wale waliokimbilia nje ya nchi wakiwa wameingia nchi jirani ya Chad.

"Awali watu waliokuwa wakikimbilia Chad walikuwa 100,000 kwa mwezi na sasa idadi imepanda hadi 245,000," alisema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya wakimbizi, Raouf Mazou.

Mapigano yasitishwa kwa sikukuu ya Eid-al-Adh'ha

Kauli hiyo ya Umoja wa Mataifa inakuja wakati Burhan na Dagalo, kila mmoja kwa upande wake, wakitangaza usitishaji mapigano kupisha maadhimisho ya Sikukuu ya Eid-Al-Adh'ha yanayofanyika leo. 

Kupitia ujumbe wa sauti uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Dagalo alisema  usitishaji huo wa mapigano ungelidumu kwa siku mbili, jana Jumanne na leo Jumatano, huku Burhan akisema kupitia hotuba yake kwenye televisheni kuwa usitishaji ni wa leo Jumatano pekee.

Sudan TRansportt eines menschen auf einer Krankenliege
Majeruhi wa vita akikimbizwa hospitalini na wauguzi mjini Khartoum.Picha: AFP

Hii na mara ya tisa kuitishwa usitishwaji mapigano tangu mzozo uanze mwezi Aprili, lakini hakuna hata mara moja ulipoheshimiwa. 

Soma zaidi:Sudan: Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano
Msafara wa ubalozi wa Marekani washambuliwa Sudan

Kwenye hotuba hiyo hiyo ya usiku wa kuamkia leo, Jenerali Burhan aliwatolea wito vijana wa Sudan kuliunga mkono jeshi ama wakiwa mahala walipo au kwa kujiunga moja kwa moja na vikosi vya serikali, katika kile alichosema ni kuilinda nchi yao.

Haikufahamika mara moja ikiwa wito wake huo ulimaanisha kuwa ni amri ya lazima kutekelezwa, kama inavyotokea kwenye mataifa yanayotumbukia vitani. 

Tamko kama hilo liliwahi kutolewa mwezi Aprili na wizara ya ulinzi ya Sudan ambayo iliwataka wanajeshi wastaafun na wa akiba kuripoti kwenye vituo cha kijeshi vilivyo karibu yao na kujiunga kwenye vita dhidi ya kundi la wanagambo wa dharura, RSF.

Vyanzo: AFP/Reuters