1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wachunguza utumwa wa ngono Sudan

19 Juni 2024

Kikosi kipya cha uchunguzi cha Umoja wa Mataifa kinachochunguza dhuluma katika vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan kimesema kinafuatilia ripoti za kutumbukizwa watu kwenye utumwa wa kingono.

https://p.dw.com/p/4hFCp
Sudan | Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Majenerali hasimu wa Sudan: Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan (kulia) na Mohamed Hamdan Dagalo.Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Vita vimeendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja kati ya jeshi la serikali linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na vikosi vya RSF vinavyoongozwa na naibu wake wa zamani, Jenerali Mohamed Hamdan Daglo.

Tume Huru ya Kimataifa ya Kutafuta Ukweli ya Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa hivi karibuni imepokea ripoti za kuaminika kuhusu matukio mengi ya unyanyasaji wa kingono yanavyofanywa na pande zinazopigana.

Soma zaidi: UN yaonya uwezekano wa janga la kibinadamu al Fashir

Mkuu wa ujumbe huo, Mohammed Chande Othman, ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba wanawake na wasichana wameendelea kukabiliwa na mateso ya kubakwa na magenge, kutekwa nyara na kuingizwa katika ndoa za kulazimishwa.

Kikosi hicho kipya cha uchunguzi cha Umoja wa Mataifa mpaka sasa kimewahoji waathiriwa wapatao 80 wakiwemo wanaume na wavulana.