1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waagiza uchunguzi wa kimataifa Ethiopia

Saleh Mwanamilongo
17 Desemba 2021

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa laagiza uchunguzi wa kimataifa kuhusu ukiukwaji wa haki katika mzozo wa Ethiopia, huku kukiwa na onyo la kutokea kwa ghasia kubwa.

https://p.dw.com/p/44UB2
UK, London | Tigray Protest
Picha: Vuk Valcic/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Akihutubia mkutano wa dharura wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, naibu mkuu wa haki za binadamu Nada al-Nashif alionya kwamba mgogoro wa kikatili wa miezi 13 wa Ethiopia katika eneo la kaskazini la Tigray unaweza kuongezeka na kuwa ghasia za jumla.

''Hatari ya kuongezeka kwa chuki, ghasia na ubaguzi ni kubwa sana, na inaweza kuenea na kuwa ghasia za jumla. Hii inaweza kuwa na athari kubwa, sio tu kwa mamilioni ya watu nchini Ethiopia, lakini pia katika kanda zima.'',alisema Nada.

Mkutano huo uliitishwa kutathmini uwezekano wa kuanzisha uchunguzi wa kimataifa kuhusu madai ya unyanyasaji wa kutisha nchini Ethiopia, yakiwemo mauaji ya maangamizi na unyanyasaji wa kijinsia.
Kikao hicho, ambacho kiliombwa na Umoja wa Ulaya kwa kuungwa mkono na zaidi ya nchi 50, kilishutumiwa na Ethiopia kuwa ni chombo cha shinikizo la kisiasa.

Soma pia:Umoja wa Mataifa kujadili hali ya haki za binadamu Ethiopia 

Wasiwasi wa Umoja wa Ulaya

Wanadiplomasia wengi walisikitishwa na ripoti za ukatili katika mzozo huo wa Tigray, ambao Umoja wa Mataifa unasema umesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha, zaidi ya watu milioni mbili kukimbia na mamia kwa maelfu kukumbwa na baa la njaa.

Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, Balozi wa Slovenia mjini Geneva alisema kwamba uzito na ukubwa wa ukiukwaji na ukatili unaofanywa dhidi ya raia kutoka pande zote, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono na kijinsia na unyanyasaji wa kikabila, haukubaliki.

Umoja huo unashinikiza kufanyika kwa uchunguzi wa kimataifa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu uliotekelezwa tangu Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutuma wanajeshi wake jimboni Tigray mwaka 2020 baada ya kukishutumu chama tawala cha eneo hilo kwa kushambulia kambi za jeshi.

Soma: TPLF waudhibiti tena mji wa Lalibela

Serikali ya Ethiopia yakosoa vikali hatua ya Umoja wa Mataifa

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliwa kwenye uwanja wa vita
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliwa kwenye uwanja wa vitaPicha: Ethiopian Prime Minister's Office//AA/picture alliance

Uchunguzi wa pamoja wa ofisi ya Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ulionya mwezi uliopita kwamba uhalifu wa kivita unawezekana unatendeka huko Ethiopia na kwamba uhalifu dhidi ya ubinadamu umefanywa na pande zote husika kwenye mzozo huo.

Ethiopia ililaani vikali wazo la kuweko na tume ya uchunguzi ya kimataifa, ikisema kwamba tayari imeshirikiana na uchunguzi wa pamoja na imeanzisha uchunguzi wake yenyewe.
Zenebe Kebede, balozi wa Ethiopia mjini Geneva alidai kuwa baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa linatumika kama chombo cha shinikizo la kisiasa, na kulenga serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.