1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasema Morocco huenda ikaomba msaada

15 Septemba 2023

Umoja wa Mataifa umesema Morocco huenda ikaomba msaada "leo au kesho" ili kuisaidia kujijenga upya kufuatia tetemeko kubwa la ardhi ambalo limeua karibu watu 3,000 na kuharibu maelfu ya makaazi ya watu.

https://p.dw.com/p/4WOEh
Picha hii ya Septemba 11,2023 inamuonyesha kijana akiwa amesimama katika mtaa mmojawapo unaokaliwa na watu wa kipato cha chini mjini Marrakech ambao umeharibiwa vibaya na tetemeko.
Picha hii ya Septemba 11,2023 inamuonyesha kijana akiwa amesimama katika mtaa mmojawapo unaokaliwa na watu wa kipato cha chini mjini Marrakech ambao umeharibiwa vibaya na tetemeko.Picha: MariaTraspaderne/Agencia EFE/IMAGO IMAGES

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura Martin Griffiths amewambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, wanataraji kujadiliana na mamlaka ya Morocco juu ya ombi la msaada ndani ya siku moja au mbili zijazo.

Morocco imeruhusu timu za uokoaji kutoka Uhispania, Uingereza, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu tangu ilipokumbwa na tetemeko la ardhi la 6.8 katika kipimo cha Ritcha Ijumaa iliyopita.

Hata hivyo, imekataa usaidizi kutoka mataifa mengine ikiwemo Marekani, Ufaransa, na baadhi ya nchi za mashariki ya kati.

Jana Alhamisi, Morocco ilitangaza kuzinduliwa kwa mpango wa msaada kwa ajili ya kuwapa makaazi mapya watu waliopoteza makao yao na kuagiza msaada wa dharura wa karibu dola elfu 3 kwa kila kaya zilizoathirika na janga hilo la kiasili.