1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

UN: Shughuli za uokozi zakaribia kumalizika Uturuki, Syria

15 Februari 2023

Umoja wa Mataifa umesema shughuli ya kuwaokoa watu waliokwama kwenye kifusi baada ya matetemko ya ardhi kuzikumba nchi za Uturuki na Syria inakaribia kumalizika.

https://p.dw.com/p/4NQZp
Türkei Syrien Erdbeben
Picha: Hiroto Sekiguchi/AP/picture alliance

Hayo yameelezwa Jumatatu na mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu na masuala ya dharura, Martin Griffiths. Akizungumza Jumatatu mjini Aleppo nchini Syria, Griffiths amesema juhudi za dharura sasa zibadili mkondo wake na zimeelekezwa zaidi kwenye kutoa misaada ya kiutu, ingawa timu za uokozi zinaendelea kuwaokoa watu wakiwa hai baada ya kukwama kwa wiki moja kwenye kifusi.

Umoja wa Mataifa umesema matetemeko hayo yaliyotokea Jumatatu iliyopita, yamesababisha vifo vya watu wapatao 35,000, huku ukisema unatarajia idadi hiyo kuongezeka na kufikia zaidi ya 50,000. Amesema jumuia ya kimataifa imeshindwa kutoa msaada wa kutosha kwa Syria, ambapo wananchi wake wamekua wakitegemea msaada wa kimataifa ambao bado haujawasili.

Watu 35,224 wamekufa 

Kulingana na takwimu za Jumamosi, watu wapatao 3,581 wamekufa nchini Syria kutokana na tetemeko hilo la ardhi, huku shirika la wafanyakazi wa uokozi wa White Helmets, wakisema watu 2,166 wamekufa katika jimbo linalodhibitiwa na waasi. Idadi ya watu waliokufa Uturuki imefikia 31,643 na hivyo kuifanya idadi jumla ya watu waliokufa kwenye nchi hizo mbili kuwa 35,224. Watu wengi walionusurika katika nchi hizo wanaishi bila ya kuwa na makaazi, karibu na mitaa ya majengo yaliyoporomoka.

Aidha, Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kiongozi wa Syria, Bashar al-Assad ameonyesha utayari wake wa kuruhusu misaada ya dharura kupelekwa kwenye maeneo ya kaskazini magharibi yanayodhibitiwa na waasi.

Türkei, Kahramanmaras | Nach dem Erdbeben
Watu waliookolewa wakipumzika kwenye mji wa Kahramanmaras, UtuturukiPicha: Suhaib Salem/REUTERS

Naye Mjumbe Maalum kwa ajili ya Syria, Geir Pedersen amesema wamesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwenye maeneo yote ya Syria, na amefurahi kuhakikishiwa hilo na serikali ya Syria kwamba itawasaidia katika kazi yao wanayoifanya nchi nzima.

''Kumekuwa na changamoto mara tu baada ya tetemeko la ardhi kutokea kuungwa mkono katika upande wa kaskazini magharibi. Tunadhani hili sasa linashughulikiwa, lakini bila shaka haliwezi kutatua matatizo yote tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Lakini sasa msaada unakuja,'' alisisitiza Perdeson.

Mtoto wa miaka 6 aokolewa

Wakati huo huo, Waziri wa Usafiri wa Uturuki, Adil Karaismailoglu amesema kuwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita anayeitwa Miray ameokolewa akiwa hai Jumatatu mchana, kutoka kwenye kifusi cha nyumba aliyokuwa akiishi kwenye mji wa Adiyaman ulioko kusini mwa Uturuki. Miray ameokolewa baada ya kukwama kwa muda wa saa 178.

Shirika la habari la CNN kupitia idhaa yake ya Kituruki, limesema kwamba timu ya uokozi pia inakaribia kumuokoa dada yake. Mapema Jumatatu asubuhi, mvulana mwenye umri wa miaka saba na mwanamke mwenye umri wa miaka 62 waliokolewa baada ya kukwama kwenye kifusi kwa takribani siku saba, katika jimbo la Hatay kusini mashariki mwa Uturuki.

Huku hayo yakijiri, wanasiasa wa upinzani wa Uturuki wameikosoa serikali ya nchi hiyo kwa kutoharakisha juhudi za uokozi. Navyo vyama vya upinzani vilivyogawanyika Jumatatu vilitarajiwa kumchagua mgombea wa pamoja atakayechuana na Rais Recep Tayyip Erdogan katika uchaguzi wa Mei, lakini mkutano huo umeahirishwa kutokana na matetemeko ya ardhi.

Nazo duru za chama tawala na zile za upinzani zinaeleza kuwa Erdogan anaweza kuuchelewesha uchaguzi huo wa rais na wabunge uliopangwa kufanyika Mei 14, kutokana na maafa makubwa yaliyosababishwa na matetemeko hayo ya ardhi.

(AFP, Reuters)