Umoja wa Mataifa na Hali ya Jamhuri ya Afrika Kati
10 Aprili 2014Ufaransa inawasilisha mswaada wa azimio unaoshauri watumwe wanajeshi elfu kumi na askari polisi 1800 watakaoshika nafasi ya wanajeshi zaidi ya elfu tano wa kikosi cha nchi za Umoja wa Afrika kinachoungwa mkono na Umoja wa mataifa MISCA. Kikosi hiki kipya cha Umoja wa mataifa kitakuwa kikijulikana kama MINUSCA na hakitarajiwi kuanza shughuli zake kabla ya Septemba 15 mwaka huu.
Mswaada huo wa azimio unaelezea hofu kubwa zilizozuka kutokana na visa vinavyokwenda kinyume na haki za binaadamu na sheria za kiutu vinavyofanywa na makundi ya wanamgambo wa zamani tangu waasi wa Seleka mpaka wa Anti Balaka, ikiwa ni pamoja na mauwaji, kamata kamata ya ovyo ovyo, mateso, ubakaji wa wanawake na watoto na wengine kutojulikana waliko.
Mswaada huo wa azimio unayataka makundi yote ya wanamgambo na waasi yaweke chini silaha, yasitishe aina zote za matumizi ya nguvu, yaache kuvuruga utulivu wa nchi na yawatoe watoto wote wanaowatumia kama wanajeshi.
Jukumu la Kikosi cha MINUSCA litakuwa kuwahifadhi raia, kulinda misaada ya kiutu, kusimamia nidhamu na utawala wa mpito pamoja na kuhakikisha haki za binaadamu zinaheshimiwa.
Kundi la kwanza la wanajeshi wa Umoja wa ulaya limeshafika Bangui
Wakati huo huo askari wa Ufaransa - Gendarme - wanaotumikia kikosi cha nchi za Umoja wa Ulaya katika Jamhuri ya Afrika kati wameshaanza kupiga doria mjini Bangui katika wakati ambapo matumizi ya nguvu yanazidi kuenea nchini humo. Watu wasiopungua 30, wengi wao wakiwa raia wameuwawa jana kufuatia mapigano kati ya wanamgambo wa kikristo Anti Balaka na wale wa kiislamu. Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Ufaransa, kundi la kwanza la wanajeshi 55 wa Umoja wa Ulaya limewasili mjini Bangui. Wiki iliyopita Umoja wa Ulaya uliahidi kutuma wanajeshi 800 katika Jamhuri ya Afrika kati hadi mwishoni mwa mwezi ujao. Bunge la Ujerumani, Bundestag, linapiga kura kuhusu kushiriki wanajeshi wa Ujerumani katika juhudi za kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika kati.
Nayo Marekani imetangaza msaada ziada wa kiutu wa dola milioni 22 kwa nchi hiyo inayosumbuliwa na kile katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon alichokiita "takasa takasa ya kikabila na kidini.
Mwandishi:Hamidou OummilkheirAP/AFP/dpa
Mhariri: Josephat Charo