1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kupiga kura kuiwekea vikwazo Syria

Isaac Gamba
28 Februari 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litapiga kura  baadaye leo (28.02.2017) juu ya rasimu ya azimio  linalolenga kuiwekea vikwazo Syria kutokana na hatua yake ya matumizi ya silaha za sumu.

https://p.dw.com/p/2YMvY
New York UN Sicherheitsrat Versammlung
Picha: Reuters/L. Jackson

Rasimu ya azimio hilo iliyoandaliwa  na Marekani, Uingereza na Ufaransa inakusudia kuwawekea vikwazo raia 11 wa Syria pamoja na taasisi 10 zinazohusishwa na mashambulizi hayo yaliyofanyika kwa kutumia silaha za sumu katika mgogoro uliochukua karibu miaka sita sasa.

Hatua hiyo pia inalenga kuzuia mauzo  ya vifaa vya kijeshi pamoja na ndege za kivita kwa jeshi la Syria au serikali ya nchi hiyo.

Pendekezo hilo linafuatia uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa uliomalizika Oktoba mwaka jana ulioihusisha Syria na matumzi ya mabomu ya mapipa kwa kutumia ndege zake za kivita kuyalenga maeneo matatu yaliyokuwa yakishikiliwa na makundi ya upinzani katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015.

Uchunguzi huo uliofanywa  na Umoja wa Mataifa ukishirikisha  shirika linalohusika na kuzuia matumizi ya silaha za sumu (OPCW) pia ulibaini  kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu lilitumia silaha za sumu katika mashambulizi yake mnamo mwaka 2015.

Balozi mdogo wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vladimir Safronkov alisema ijumaa iliyopita kuwa  Urusi itatumia kura yake ya turufu kupinga hatua hiyo kwa sababu imeegemea upande mmoja  na hakuna  ushahidi wa kutosha.

 

Syria yakanusha matumizi ya silaha za sumu

Syrien Konflikt Idlib
Mji wa jimbo la Kaskazini wa Idlib nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/G. Omran

Serikali ya Syria imekuwa ikiendelea kukanusha matumizi ya silaha za sumu katika vita nchini humo ambayo tayari imewaua watu 310,000 tangu ilipoibuka Machi 2011.

Wakati huohuo mashambulizi ya anga yaliyofanywa katika jimbo la Idlib hapo jana  yamewaua kiasi ya watu 11 na kutia doa mazungumzo ya amani ya Syria  yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Geneva yakishirikisha upande wa serikali na makundi ya waasi.

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazodai kuuawa  afisa wa juu wa kundi la itikadi kali la al-Qaeda katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa katika jimbo la Idlib.

Kundi la Ujasusi la SITE linalofuatilia makundi ya itikadi kali limesema Abdullah Muhammad Rajab Abdulrahman ambaye ni kiongozi msaidizi wa kiongozi wa al-Qaeda Ayman al-Zawahiri anaweza kuwa ameuawa katika mashambulizi hayo yaliyofanywa na ndege za kivita za Marekani.

Jimbo la kaskazini mashariki linadhibitiwa zaidi na kundi la al-Qaida lenye mafungamano na kundi la waasi ambako mamia ya raia wa Syria waliolazimika kuhama maeneo yao ya makazi wanaishi kama wakimbizi katika eneo hilo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/APE

Mhariri : Iddi Ssessanga