1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika waelekea kupendekeza mjadala juu ya Zimbabwe

Nijimbere, Gregoire30 Juni 2008

Wakati nchi nyingi za magharibi na hususan Marekani zinapendekeza kuiwekea vikwazo serikali ya rais Robert Mugabe, inaelekea Umoja wa Afrika unataka njia ya majadiliano kufikia maridhiano ya kitaifa nchini Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/ETh7
Rais Robert Mugabe katika mkutano wa Charm el-Cheikh MisriPicha: AP

Kufanyika duru ya pili ya uchaguzi baada ya kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kujitoa akilalamika juu ya mashambulizi dhidi ya wafuasi wake kulilaaniwa na jamii ya kimataifa na hususan nchi za magharibi na Umoja wa mataifa. Lakini kwenye Umoja wa afrika, pamoja na kuendelea lawama hizo, juhudi zinaelekea kutuliza hali ya mambo nchini Zimbabwe badala ya vuta ni kuvute.

Wakati wa hotuba za ufunguzi mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika, kamishena wa Umoja wa Afrika ni miongoni mwa waliopewa nafasi kuzungumza.

Jean Ping amesema na hapa ninamnukuu´´ningependelea kuona bara la Afrika linachukuwa jukumu lake na kufanya kila liwezalo ili pande zinazohusika na mzozo nchini Zimbabwe ziweze kushughulika pamoja na kuyasuluhisha matatizo yao``.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa´mataifa Asha Rose Migiro, kwa upande wake ametoa kauli kama hiyo ila yeye jukumu kubwa ameliweka mikononi mwa viongozi wa kiafrika: ´´Inasikitisha kuona kuwa uchaguzi uliendelea licha ya wasi wasi ulioelezewa na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa mataifa na kutaka uchaguzi huo usimamishwe. Huu ni mtihani kwa viongozi wa kiafrika.

Wengi walitoa sauti zao kuhusu swala hilo.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anawasihi, waheshimiwa, msaidieni haraka lifikiwe suluhu kupitia mazungumzo´´.


Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, kwa upande wake ameiomba jamii ya kimataifa kushirikiana na jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa ASfrika SADC katika juhudi za kulitafutia suluhu swala la Zimbabwe.


Wakati rais Robert Mugabe akiwasili nchini Misri jana jioni baada ya kuapishwa kuiongoza nchi kwa mhula mwingine wa miaka mitano ijayo, Afrika ya kusini, msuluhishi katika mgogoro huo wa Zimbabwe, ilitoa mwito kwa chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF na chama cha upinzani cha mageuzi ya kidemokrasi MDC cha Morgan Tsvangirai kuzungumza.

Na zaidi ya hayo na kwa mara ya kwanza rais wa Afrika ya kusini Thabo Mbeki katika taarifa aliyoitoa amependekeza kuundwa kwa serikali ya mpito na wazo hilo limeungwa mkono na Ethiopia.

Msimamo huo pamoja na mazungumzo wakati ya maandalizi, yanayonyesha kuwa Umoja wa Afrika unapendelea kufikiwe suluhu kupitia njia ya mazungumzo badala ya kuiwekea serikali ya rais Mugabe vikwazo kama inavyoombwa na nchi za magharibi. Tayari mkuu wa idara ya ulinzi kwenye Umoja wa Afrika alitupilia mbali pendekezo la kukituma kikosi cha kijeshi cha kulinda amani nchini Zimbabwe kama inavyodaiwa na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai bila kuweko mkataba wa amani.