Umoja wa Afrika waandaa "ramani ya amani", waasi wamkana Gaddafi
11 Aprili 2011Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen, ameeleza kuwa hakuna suluhisho la kijeshi katika mgogoro wa Libya.
Kiongozi wa Libya Kanali Gaddafi pia angelipendelea kuona mapigano yakisimamishwa lakini kwa sharti kwamba wapinzani wake hawatoi masharti.
Lakini kwa wapinzani, kuendelea Gaddafi kuwamo madarakani siyo jambo linaloweza kueleweka asilani.
Jee wapinzani wa Libya wanataka nini.?
Wajumbe wa jumuiya ya kutetea demokrasia wamekutana kwa mara ya kwanza nchini Libya na kujadili shabaha wanazozilenga, ikiwa pamoja na kuanzishwa mfumo wa uwakilishi wa bunge, kuandikwa katiba ya kitaifa, kuleta uhuru wa vyombo vya habari na uhuru kwa ajili ya wanawake na kushirikishwa wanawake hao katika nyanja zote za kijamii.
Wawakilishi wa jumuiya ya watetea demokrasi wamekutana katika mji wa Benghazi kujadili mustakabali wa Libya wakati ambapo ndege za NATO zinaendelea kufanya mashambulio na wakati ambapo ujumbe wa nchi za Umoja wa Afrika unatarajiwa kufanya mazungumzo na wapinzani katika mji huo wa Benghazi. Lengo la ujumbe huo ni kutafuta suluhisho la amani nchini Libya
Ujumbe huo unaoongozwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, umeshakutana na utawala wa Gaddafi. Rais Zuma ameeleza kuwa serikali ya Kanali Gaddafi imeukubali mpango wa amani uliowasilishwa na Umoja wa Afrika.
Hata hivyo, wapinzani wa Gaddafi wanaokutana kwenye kongamano linalofafanua mustkabali wa Libya, wamesema wanapendelea watu wasema kuwa Libya imekombolewa na watu wa Libya wenyewe.
Wakati mapambano makali yanaendelea katika miji ya Adjabiya na Misrata baina ya majeshi ya Gaddafi na ya waasi, uzalendo unasisitizwa kwenye kongamano la mjini Benghazi kuwa msingi wa kuleta suluhisho nchini Libya
Hayo ameyasisitiza pia Esraa, dada mwenye umri wa miaka 20 aliyewahi kuishi nje ya Libya kwa muda mrefu. Dada huyo anatakakusikia watu wakisema kuwa Libya imekomboleewaa na watu wa Libya wenyewe.
Mwandishi: Esther Saoub/ÜSWR
Tafsiri: Abdou Mtullya
Mhariri: Josephat Charo