1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulipaji kodi ya majengo nchini Tanzania wazua malalamiko

Deo Kaji Makomba
20 Agosti 2021

Tanzania imeanza utekelezaji wa makusanyo ya kodi ya majengo baada ya mpango huo kupitishwa na bunge,hata hivyo hatua hiyo imeibua malalamiko kutoka kwa watu.

https://p.dw.com/p/3zG9x
Tansania Feuer auf dem Kilimandscharo
Picha: Jaysadventure/Reuters

Kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa ulipaji kodi ya majengo nchini Tanzania kwa njia ya luku kumeibua hisia mseto huku baadhi ya watu wakisema kuwa kodi hiyo ilipaswa kulipwa na wamiliki wa nyumba na wala sio wapangaji.

Kulingana na maamuzi yaliyopitishwa na bunge la bajeti lililopita ulipaji wa kodi ya majengo utafanyika kwa njia ya mfumo wa ununuaji umeme ambapo sasa kila mwananchi anayenunua umeme kwa mfumo huo atakakuwa akikatwa kiasi cha pesa kwa ajili ya kodi hiyo. 

Suala la mzigo wa kodi kutupiwa watu wenye kipato cha chini ndio mjadala mkubwa unaozungumziwa hivi sasa nchini Tanzania, watu wakihoji ni vipi serikali kupitia bunge walipitisha mfumo huo wa ulipaji kodi ambao unaonekana kuwakandamiza watu wa kipato cha chini. 

Nani atakiwa kulipa tozo za nyumba ?

Tansania Dar es Salaam | Grafitty zu Corona
Picha: Eric Boniphace/DW

Eddy Mbaya ni mkaazi wa Nyakato National Jijini Mwanza na Maguye Simioni mkaazi wa Morotonga Wilayani Serengeti mkoani Mara wanasema. 

''Kwa maoni yangu mimi kuhusu hiyo kodi,anaye takiwa aliilipe ni mwenyi nyumba na sio wapangaji'', alisema Mbaya.

Wengi wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa suala hili litaleta utata mkubwa kwa wananchi wa kawaida. Gwandumi Mwakatobe ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa akiwa Sumbawanga mkoani Rukwa. 

''Nchi hii ingekuwa na wapangaji wa chache au kila mtu angekuwa na nyumba hapo kodi hiyo inge eleweka, kwamba kodi imeongozewa kwa watu wanaotumia umeme katika nyumba zao.'', alisema Mwakatobe.

Hadi hivi sasa watu mbalimbali nchini Tanzania wako njia panda huku wakiendelea kuwa na maswali ya ni kwa nini mwenye nyumba alipiwe kodi ya jengo?