1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wasubiri mkataba wa COP26

13 Novemba 2021

Wawakilishi wa mataifa duniani wanaokutana mjini Glasgow kwa mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa COP26 wametumia siku ya Jumamosi kupigania uwezekano wa kufikia mkataba.

https://p.dw.com/p/42xYt
UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow I Protest
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Kwa karibu siku nzima wajumbe hao wamekuwa wakijadili mapendekezo mapya yanayonuwia kupatikana kwa mkataba utakaotanua juhudi za ulimwengu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Maafisa wa Uingereza wanaoongoza majadiliano mjini Glasgow, Scotland walitoa rasimu mpya makubaliano baada ya juhudi chungunzima za kidiplomasia zilizoendelea hadi siku ya Ijumaa ambayo ndiyo ilikuwa ya mwisho ili kufikiwa makubaliano.

Mjumbe wa Marekani kuhusu mabadiliko ya tabianchi John Kerry na mwenzake wa China, Xe Zhenhua, wote wameonesha mashaka juu ya iwapo majadiliano hayo yaliyorefushwa yatazaa matunda.

Kibarua bado ni kigumu kufikia makubaliano 

Kwa jumla moja ya changamoto kubwa ni lugha iliyotumika kwenye baadhi ya mapendekezo ikiwemo lile la kuyataka mataifa kuongeza juhudi "kuelekea kuachana na matumizi ya makaa ya mawe na kutoa ruzuku kwa shughuli za utafutaji na uchimbaji mafuta"

UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow I PK
Picha: Yves Herman/REUTERS

Lakini kwenye pendekezo la nyongeza, aya moja wapo inatambua umuhimu wa kuwa na kipindi cha mpito kitakachowezesha wale waliowekeza na kufanya kazi kwenye sekta ya mafuta wapatiwe msaada wa kifedha wanapoelekea kuachana na shughuli hiyo.

Alok Sharma, afisa wa Uingereza anayeongoza majadiliano hayo ya mjini Glasgowa amesema ana matumaini kuwa mataifa yatafikia makubaliano ya maana kwenye saa za lala salama huko Scotland.

"Nina matumaini tutafikia malengo" amesema Sharma, alipozungumza na  shirika la habari la Asosciated Press mapema siku ya Jumamosi.

Baadhi ya makundi ya wanaharakati wa mazingira yamesema mapendekezo yaliyo mezani hivi sasa kwa wajumbe kuamua hayana uzito wa kutosha.

 "Hapa Glasgow, mataifa masikini duniani yamo kwenye hatari yakupoteza sauti kwenye majadiliano haya lakini saa chache zijazo zinaweza na ni lazima zitumike kubadili mwelekeo" amesema Tracy Carty, mshauri mwandamizi wa masuala ya kisera wa shirika la Oxfam.

Suala la fedha kwa mataifa masikini bado kizungumkuti 

Lakini licha ya hayo uwezekano wa kutajwa kwa mara ya kwanza suala la nishati ya mafuta kwenye mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi kwa sehemu fulani umepokelewa vyema na baadhi ya wanaharakati wa mazingira.

"Bado ni dhaifu na inatia wasiwasi, lakini tunaliona suala hilo kuwa hatua muhimu sana" amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la masuala ya mazingira la Greenpeace, Jennifer Morgan.

UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow I Protest
Picha: Andy Buchanan/AFP

Amesema itafaa wapambane sana kuhakikisha kipengele kuhusu umuhimu wa kuachana na nishati ya mafuta kinabakia kwenye mkataba na kinaboroshwa katika saa za mwisho za majadiliano.

Migawanyiko bado imesalia kwenye suala la msaada wa kifedha unaopigiwa upatu na mataifa masikini.

Marekani na Umoja wa Ulaya zinazoongoza kwa utoaji wa gesi ya Ukaa bado wanajivuta vuta kukubaliana na madai ya nchi masikini yanayosema iwapo msaada wa kifedha hautapatikana, yatakabiliwa na athari zisizo kifani miaka michache inayokuja.

Mwandishi: Rashi Chilumba

Mhariri: Yusra Buwahyid