1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yawasilisha rasimu ya maazimio IAEA kuhusu Iran

4 Juni 2024

Mataifa ya Ulaya Ujerumani, Uingereza na Ufaransa zimewasilisha rasimu pana ya maazimio dhidi ya Iran katika bodi kuu ya Umoja wa Mataifa inayosimamia zana za nyuklia, ili iweze kupigiwa kura wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/4gbqI
Isfahan, Iran | Nishati ya Atomiki | Rafael Grossi akiwa na Mohammad Eslami
Mkuu wa shirika la IAEA Rafael Grossi akiwa na Mohammad Eslam Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki Iran.Picha: Tasnim

Haya ni kulingana na waraka ulioonekana na shirika la habari la Reuters. Waraka huo unakuja baada ya azimio lililopitishwa miezi 18 iliyopita lililoiamrisha Iran kutoa ushirikiano kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la IAEA katika uchunguzi wake kuhusiana na chembechembe za urani zilizopatikana katika maeneo ambayo hayakuwekwa wazi nchini Iran.

Soma pia:Iran yasema mazungumzo na mkuu wa IAEA yalikuwa mazuri

Waraka huo pia unazungumzia matatizo yaliyoibuka hivi karibuni kama Iran kuwazuia wataalam wakuu wa shirika la IAEA katika masuala ya urutubishaji wa urani, waliokuwa katika kikosi kinachofanya uchunguzi.

Tangu mwaka 2022, maeneo yanayodaiwa kuwa na chembechembe hizo za urani na yanayochunguzwa yamepungua kutoka matatu hadi mawili ila Iran bado haijaelezea ni wapi zilipotokea chembechembe hizo za urani.