1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya na China zatarajia mwanzo mpya wa mahusiano

6 Aprili 2023

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kiongozi wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Urusula von der Leyen wako Beijing katika ziara ya kipekee

https://p.dw.com/p/4Plna
China Peking | Treffen Präsident Emmanuel Macron und Premierminister Li Qiang
Picha: Thibault Camus/AP Photo/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen wameanza mkururo wa mikutano na viongozi wa China mjini Beijing yatakayojikita kwenye masuala mbalimbali ikiwemo vita nchini Ukraine.

Frankreich | Emmanuel Macron und Ursula von der Leyen in Paris
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais wa Ufaransa baada ya kuwasili Beijing Jumatano jioni alisema Ulaya inapaswa kujiepusha kupunguza mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia na China lakini pia akapinga kile ambacho baadhi ya watu wanakizungumzia kuwa ni mzunguuko usioepukika wa mivutano kati ya China na nchi za Magharibi.

Leo Alhamisi, rais huyo amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa China Li Qiang kabla ya kukaa na rais Xi Jingping pamoja na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen kwa mazungumzo ambayo yanaweza kuanzisha enzi mpya ya mahusiano kwa jumuiya hiyo na China baada ya miaka ya mahusiano ya mivutano.

Kabla ya mkutano huo rais Macron amemtolea mwito kiongozi wa China Xi Jingping kuzungumza na Urusi kujaribu kumaliza vita nchini Ukraine. Mwito huo ameutowa muda mfupi wakati akiwa amesimama pamoja na mwenyeji wake huyo nje ya ukumbi wa bunge la umma wa China, kabla ya mkutano wao wa kwanza.

China Peking | Xi Jinping und Emmanuel Macron
Picha: Thibault Camus/AP Photo/picture alliance

Rais Macron alisema anaamini masuala mbali mbali yatajadiliwa kwenye mkutano huo.Viongozi wa EU kujadili ulinzi,China na Marekani

Awali pia waziri mkuu wa China Li Qiang alikutana vile vile na mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya  von der Leyen ambaye hata kabla ya ziara yake hiyo ya kwanza China tangu alipochukua uongozi wa Jumuiya hiyo mwaka 2019, alisema Ulaya inapaswa kutohatarisha mahusiano yake ya kidiplomasia na kiuchumi na nchi hiyo ya China.

Kiongozi huyo alisema Ulaya na China  zote zimefaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na mahusiano yao ingawa mahusiano hayo yamekuwa yakiandamwa na matatizo katika miaka ya hivi karibuni na ni muhimu yawepo majadiliano kwa pande zote juu ya masuala yote yaliyopo kwenye mahusiano ya pande hizo mbili kwa hivi sasa.

Waziri mkuu wa China Li Qiang kwa upande wake ameweka wazi kwamba mahusiano baina ya nchi yake na Umoja wa Ulaya na Ufaransa iko kwenye nafasi ya kufungua ukurasa mpya na pande zote zinapaswa kuzingatia mwelekeo wa kuheshimiana na ushirikiano utakaozifaidi pande zote.Viongozi wa dunia wailaani Urusi kuhusu Ukraine

EU Die Präsidentin der Europäischen Kommission Ursula von der Leyen hält eine Grudsatzrede zu den Beziehungen zwischen der EU und China
Picha: Valeria Mongelli/AFP

Mahusiano ya Ulaya na China katika miaka ya karibuni yalizidi kuwa mabaya kutokana na masuala kadhaa ikiwemo madai kwamba China inakiuka haki za binadamu katika mkoa wa Xinjiang,kukwama kwa mpango wa uwekezaji, lakini pia ikikosolewa kwa kushindwa kuwa wazi katika suala la janga la Uviko-19, kadhalika kutokana na msimamo wake wa kushindwa kuilaani Urusi juu ya uvamizi wake nchini Ukraine.

China lakini kwa upande wake inashauku kubwa hivi sasa kuhakikisha kwamba Ulaya haifuati kile inachokiona kama juhudi zinazoongozwa na Marekani za kutaka kudhibiti ukuaji wake. Na inavyoonesha alau kuna matumaini ya kupatikana mwafaka wa kuondowa migawanyiko na Ufaransa.

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW