1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabilioni ya dola kuziokowa chumi dhidi ya corona

18 Machi 2020

Marekani na Ulaya zinaripotiwa kuingiza mabilioni ya dola kuziokowa chumi zilizoelemewa na janga la kirusi cha corona, huku Umoja wa Ulaya ukifunga mipaka kwa siku 30 wakati idadi ya maambukizi mapya yakishamiri.

https://p.dw.com/p/3Zcu6
Arcturus Therapeutics, ein Unternehmen für RNA-Arzneimittel, erforscht einen Impfstoff gegen das neuartige Coronavirus (COVID-10)
Picha: Reuters/B. Guan

Rais Donald Trump wa Marekani alisema hapo jana (Jumanne 17 Machi) kwamba atapeleka mbele ya baraza la Congress mswada wa sheria ambayo inajumuisha malipo ya fedha taslimu kwa mamilioni ya Wamarekani. Gazeti la The Washington Post linasema zinaweza kufika dola bilioni 850, sehemu kubwa ikielekezwa kwa mashirika ya ndege ambayo yanahofia kusambaratika.

Hali ni kama hiyo nchini Uingereza, ambako Waziri wa Fedha Rishi Sunak amezinduwa mpango wenye thamani ya paundi bilioni 330 kwa ajili ya kampuni zinazokaribia kufilisika kutokana na athari za kirusi cha corona. 

Kwa upande wake, Ufaransa imeahidi kutowa euro bilioni 45.

Hatua hizi za jumla jamala zisizowahi kushuhudiwa popote katika wakati wa amani zimewashituwa watu ulimwenguni kote na kuyafanya masoko ya fedha yatikisike kwa khofu ya mserereko wa kiuchumi unaotazamiwa muda wowote kuanzia sasa. 

Uturuki yapoteza mtu wa kwanza kwa corona

Türkei Corona-Krise | Istanbul
Watu wakiwa wamevaa vizibo vya kujilinda na maambukizi ya kirusi cha corona mjini Istanbul, huku Uturuki ikisema mmoja kati ya wagonjwa 98 wa COVID-19 amefariki dunia.Picha: AFP/O. Kose

Haya yanajiri huku Uturuki, taifa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, ikitangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa COVID-19, miongoni mwa watu 98 waliokwishagunduliwa na kirusi hicho hadi sasa.

Waziri wa Afya wa Uturuki, Fahretttin Koca, amewaambia waandishi wa habari kwamba mgonjwa huyo alikutana na watu waliotoka China.

"Kwa mara ya kwanza kwenye mapambano yetu dhidi ya kirusi hiki, leo nimempoteza mgonjwa mmoja. Binafsi nilikuwa mmoja wa waliokuwa wakimfuatilia kwa ukaribu sana. Alikuwa na umri wa miaka 89. Leo pekee watu wengine 51 wamekutwa na kirusi hicho, na hivyo idadi ya wagonjwa imefikia 98. Lakini wengi wao wameanza kupona," alisema Fahrettin.

Limbourg naye agunduliwa na corona

Intendant Peter Limbourg, Pressebild.
Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter LimbourgPicha: DW/J. Röhl

Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter Limbourg, amekuwa mtu wa karibuni kabisa kujitangaza kwamba naye ameambukizwa kirusi hicho cha corona.

Kwenye taarifa yake, Limbourg amesema alipata majibu ya vipimo vyake jioni ya jana, na kwamba tangu wakati huo yuko kwenye karantini, akifanyia kazi zake akiwa nyumbani.

Watu wote waliokuwa karibu yake nao wamechukuliwa vipimo huku taratibu za kiafya zikiendelea.

Wakati huo huo, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amethibitisha marufuku ya siku 30 kuwazuwia watu kuingia kwenye mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Kwa ujumla mataifa ya Umoja huo yanakaribia kuwamo kwenye karantini ya jumla, ambapo nchi ya karibuni kabisa kutangaza ni Ubelgiji hapo jana, itakayoendelea hadi tarehe 5 Aprili.

Hatua hii, ambayo wengine wanahoji kuwa imechelewa, imepongezwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO.

Nchini Australia maambukizi yamefikia 565, huku serikali ikiwataka raia kutosafiri kwenda nje na kutokushiriki kwenye mikusanyiko inayozidi watu 100. 

Afrika, ambayo ina mifumo dhaifu ya afya, imeripoti wagonjwa 400 hadi sasa, huku Amerika Kusini ikithibitisha zaidi ya watu 1,100 walioambukizwa.