1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuendelea kujipanua

6 Oktoba 2021

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema tume yake itaendelea kufanya kila linalowezekana kuuendeleza mchakato wa upanuzi wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/41Lf2
Slowenien l Westbalkan-Gipfel der EU in Brdo
Picha: Joe Klamar/AFP

Umoja huo umesema unaendelea na majadiliano na wanachama wake 27 kuhusiana na iwapo utaendelea kuwapokea wanachama wapya. 

Ursula von der Leyen amewaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wa kilele unaohusiana na masuala ya Balkani Magharibi, amerudia matamshi yake kwamba wanataka mataifa ya eneo hilo kujiunga na Umoja wa Ulaya, lakini pia kutimiza lengo lao kubwa la kuupanua umoja huo.

Mapema, rais wa baraza la umoja huo Charles Michel aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba bado majadiliano yanaendelea baina yao na mataifa wanachama kuhusiana na uwezo wa jumuiya hiyo kuchukua wanachama wapya.

Michel amesema wanaangazia uwezo wa kuongeza wanachama wapya baada ya mkutano huo wa kilele kati ya mataifa ya Balkani na viongozi hao nchini Slovenia.

Amesema "Kwa upande mwingine, itakuwa pia ni fursa ya kuhakikisha kwamba tupo tayari kuhamasisha upatikanaji wa fedha zaidi ili kuwekeza nchini humo na kusaidia mabadiliko na mapambano dhidi ya ufisadi na kuhamasisha utawala bora. Tunataka kushirikiana kwa karibu na mataifa hayo na hii itakuwa ni fursa ya kubadilishana mawazo kwa uwazi ili kung'amua awamu zinazofuata."

Angela Merkel beim Balkan-EU_Gipfel in Slowenien
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema hakuna sababu ya kuweka muda wa kuwakubali waombaji wapya kwenye Umoja wa Ulaya.Picha: Petr David Josek/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kwa upande wake amekataa wito wa kupanga tarehe rasmi kwa mataifa hayo ya Balkan kukubaliwa uwanachama wa Umoja huo. Merkel amesema haamini katika kupanga tarehe bali anaamini katika kutekeleza ahadi zao na kuongeza kuwa watakapokidhi vigezo vitakapokidhi wataweza kujiunga.

Juu ya hayo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kmataifa hayo yako katika mkondo wa kujiunga na Umoja huo lakini ni muhimu yakawekewa mazingira yanayostahili uwekezaji na biashara na hatimaye kuwa mwanachama.

Albania na Macedonia ya Magharibi tayari wamekidhi vigezo vya kuanza mazungumzo, lakini mataifa wanachama yatatakiwa kuridhia kwa pamoja kuendeleza mchakato huo. Nchi mwanachama Bulgaria inapinga Macedonia kukubaliwa kwa sababu ya mzozo wa utambulisho wa lugha na utaifa.

Aidha wakuu hao wamezungumzia kupanda kwa gharama za nishati, huku kukitolewa mwito kwa umoja huo kuwahimiza wanachama wake kutoa mikopo nafuu kwa watumiaji na biashara ndogondogo zilizoathirika zaidi na ongezeko la gharama za gesi huku ukosoaji ukiongezeka dhidi ya umoja huo kwamba sera zake juu ya mabadiliko ya tabianchi zinachochea matatizo.

Mashirika: RTRE