1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Ulaya haijafikia makubaliano juu ya nafasi ya von der Leyen

18 Juni 2024

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesema kuwa viongozi wa umoja huo bado hawajafikia uamuzi kuhusu muhula wa pili kwa Ursula von der Leyen kuhudumu kama Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/4hAzk
Schweiz Gipfeltreffen zum Frieden in der Ukraine
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen Picha: EPA/Denis Balibouse

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amewaambia waandishi wa habari kuwa, licha ya kuwepo matarajio ya kufikiwa makubaliano kuhusu nafasi hiyo, uamuzi wa mwisho bado haujatolewa.

Ameonyesha matumaini kuwa makubaliano huenda yakafikiwa wiki ijayo.

Soma pia: Scholz amuonya von der Leyen kutoshirikiana na vyama vya itikadi kali

Wakikutana kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi wa bunge la Ulaya, huku vyama vya kizalendo na vile vya siasa kali za mrengo wa kulia vikipata mafanikio makubwa Ufaransa na Ujerumani, viongozi wa Ulaya wamejadili jinsi ya kujaza nafasi kuu za baraza lijalo la Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa zamani wa Ureno António Costa anapigiwa upatu kuchukua nafasi ya Charles Michel kama Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya na kutwikwa jukumu la kuleta maelewano kati ya viongozi wa Ulaya naye Waziri Mkuu wa Estonoa Kaja Kallas akitazamiwa kurithi nafasi ya mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, inayoshikiliwa na Josep Borell.