1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yatuma tena ndege zisizo rubani ndani ya Urusi

26 Desemba 2022

Urusi inasema imeidungua ndege isiyo rubani kutoka Ukraine ambayo ilikuwa inakaribia kwenye kwenye kituo chake cha jeshi la anga cha Engels kilicho ndani kabisa ya Urusi, hali inayoashiria uwezo duni wa kujilinda.

https://p.dw.com/p/4LQjO
Russland Russische Militärübungen
Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Hii ni mara ya pili kwa kituo hicho cha jeshi la anga la Urusi kuwa shabaha ya mashambulizi ya Ukraine katika mwezi Disemba, hali inayozusha masuala juu ya uwezo wa mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi, ikiwa ndege zisizo rubani zinaweza kuruka hadi ndani kabisa ya mamlaka yake.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema tukio hilo lilitokea mapema siku ya Jumatatu (Disemba 26) ambapo wanajeshi wake watatu waliuawa kutoka na mabaki ya ndege hiyo isiyo rubani kwenye kituo cha jeshi la anga cha Engels ambacho kinahifadhi ndege mbili zenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia, Tu-95 na Tu-96. 

Kituo hicho cha kijeshi kilicho kwenye mkoa wa Saratov karibu na Mto Volga, umbali wa kilomita 600 mashariki mwa mpaka na Ukraine, kimekuwa kikitumika kufanyia mashambulizi dhidi ya Ukraine.

Kwa mujibu wa wizara hiyo ya ulinzi, hakuna ndege yoyote ya Urusi iliyoathirika kwa mashambulizi hayo.

Mara ya pili kushambuliwa

Hii ni mara ya pili kwa kituo cha jeshi la anga cha Engels kulengwa na ndege zisizo rubani za Ukraine, mara kwanza ikiwa Disemba 5, ambapo mashambulizi dhidi ya kituo hicho na chengine cha Dyagilevo kilicho jimbo la Ryazan magharibi mwa Urusi yaliuwa wanajeshi watatu kuwajeruhi wengine wanne.

Russland Luftwaffenstützpunkt Engels in Saratow
Kituo cha jeshi la anga cha Engels.Picha: Maxar Technologies/REUTERS

Mashambulizi hayo yalifuatiwa na makombora kadhaa ya kulipiza kisasi kutoka Urusi ambayo yalipiga nyumba na majengo na kuuwa raia kadhaa nchini Ukraine.

Nchini Ukraine, usiku wa kuamkia Jumatatu ulishuhudia utulivu usio wa kawaida, ambapo kwa mara ya kwanza vikosi vya Urusi havikuushambulia mkoa wa  Dnipropetrovsk unaopakana na mikoa miwili ya kusini ya Khersonna Zaporizhzhia, kwa mujibu wa gavana wa mkoa huo, Valentyn Reznichenko.

Urusi yapunguza mashambulizi 

"Huu ni usiku wa tatu mtulivu ndani ya miezi mitano na nusu tangu Warusi waanze mashambulizi yao dhidi ya mji wa Nikopol," aliandika gavana huyo. Nikopol iko karibu na Mto Dnieper, umbali mdogo kutoka kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na vikosi vya Urusi.

Russland Präsident Putin besucht Rüstungsfirma Shcheglovsky Val
Rais Vladimir Putin wa Urusi (katikati) akiwa na washirika wake serikalini.Picha: Russian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

Maeneo yanayodhibitiwa na Ukraine kwenye mkoa jirani wa Kherson yalishambuliwa mara 33 ndani ya kipindi cha masaa 24, kwa mujibu wa gavana wa mkoa huo anayeelemea upande wa Ukraine, Yaroslav Yanushevich, ambaye pia alithibitisha kutokuwa na kifo wala majeruhi yeyote.

Siku ya Jumamosi (Disemba 24) mashambulizi makali kabisa katika mji wa Kherson, uliotwaliwa tena na vikosi vya Ukraine mwezi Novemba, yaliuwa na kujeruhiwa watu kadhaa.