1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yasema wanajeshi wake wanasonga mbele Bakhmut

12 Mei 2023

Ukraine inasema imepiga hatua kubwa kwenye mapambano ya kuwania udhibiti mji wa Bakhmout na huku kundi la wanajeshi mamluki la Wagner likimtaka waziri wa ulinzi wa Urusi kuuzuru mji huo kutathmini hali ya mambo.

https://p.dw.com/p/4RGBl
Ukraine Bachmut Luftaufnahme Zerstörung
Picha: Libkos/AP Photo

Wizara ya Ulinzi ya Ukraine ilisema siku ya Ijumaa (Mei 12) kwamba wapiganaji wake wamepata mafanikio makubwa karibu sana na mji unaowania wa Bakhmut ulio kwenye jimbo la mashariki la Donetsk. 

Ujumbe uliotumwa kwa njia ya Telegram na naibu waziri wa ulinzi, Hanna Miliar, ulisema: "Walinzi wetu wamesonga mbele kwa kilomita mbili ndani ya Bakhamut."

Naibu waziri huyo wa ulinzi alisema wanajeshi wa Ukraine hawajaondoka kutoka sehemu yoyote ya mji huo kwa wiki nzima sasa na badala yake jeshi la Urusi limepata hasara kubwa.

Soma zaidi: Mapigano makali yaendelea Bakhmut huku kila upande ukidai mafanikio

Awali, waandishi wa habari za vita wa Urusi walikuwa wameripoti juu ya kusonga mbele kwa majeshi ya Ukraine kwenye eneo la mstari wa mbele wa mapigano mjini Bakhmut.

Mzozo baina ya Wagner na wizara ya ulinzi ya Urusi

Hata hivyo, mkuu wa kundi la wanajeshi wa kukodi la Urusi la Wagner, Yevgeny Prigozhin, alidai kuwa wapiganaji wake ndio waliokuwa wakisonga mbele ingawa kwa kasi ndogo.

Ukraine Bakhmut Grad Raketenwerfer
Makombora yakirushwa baina ya wanajeshi wa Ukraine na Urusi katika mji wa Bakhmut.Picha: Ukraine Armed Forces via REUTERS

Mkuu huyo wa Wagner alimtolea wito waziri wa ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, kuutembelea mji huo kujionea mwenyewe kinachoendelea. 

"Kutokana na hali ngumu ya operesheni hii na uzoefu wako wa miaka mingi wa kijeshi, nakuomba uje Bakhmut, ambayo inamilikiwa na vikosi vya kijeshi vya Urusi, kutathmini hali hii mwenyewe." Aliandika Prigozhin kwenye barua ya wazi kwa Shoigu. 

Soma zaidi: Duru zadokeza Zelensky kuitembelea Italia mwishoni mwa juma

Wanajeshi wa Urusi wanadhibiti asilimia 95 ya Bakhmut, mji uliowahi kuwa na wakaazi 700,000, na ambao kwa sasa takribani umeharibiwa kabisa na mapigano ya miezi kadhaa. 

Mahusiano baina ya vikosi vya Wagner na wizara ya ulinzi ya Urusi yamekuwa ya mashaka, huku Prigozhin akilalamikia ukosefu wa silaha wa kutosha na mara kadhaa akimshambulia waziwazi waziri huyo wa ulinzi, ambaye ana cheo cha jenerali wa jeshi, hakuwahi kuhudumu jeshini hata mara moja.  

China yajitosa kusaka amani

Bildkombo Selenskyj und Xi Jinping
Rais Ji Xinping wa China (kushoto) na Rais Volodymr Zelensky wa Ukraine.Picha: Ukrainian Presidentia/IMAGO/MONCLOA PALACE/REUTERS

Hayo yakijiri, China inamtuma mjumbe wake wa ngazi za juu katika mataifa ya Ukraine, Poland, Ujerumani, Ufaransa na Urusi kujaribu kuanzisha mazungumzo ya amani kwa vita ambavyo vinaendelea nchini Ukraine.

Li Hui, ambaye ni mjumbe maalum anayehusika na mataifa ya Eurasia, ataanza ziara yake siku ya Jumatatu (Mei 15) akiwa na jukumu la kuanzisha majadiliano ya kisiasa kuutatuwa mzozo huo. 

Kutumwa kwake kunafuatia mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya simu kati ya Rais Ji Xinping wa China na Rais Volodymr Zelensky wa Ukraine wiki mbili zilizopita.

Vyanzo: Reuters, dpa