1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Poroshenko asema bado Ukraine haijafikia kupiga goti

Mjahida24 Agosti 2016

Rais Petro Poroshenkowa Ukraine ameishutumu Urusi kwa uvamizi, wakati taifa hilo likiadhimisha miaka 25 ya uhuru wake.

https://p.dw.com/p/1Jp47
Rais Petro Poroshenko akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Uhuru wa Ukraine
Rais Petro Poroshenko akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Uhuru wa UkrainePicha: Reuters/G. Garanich

"Sasa nawaalika kunyamaza kimya kwa dakika moja kwa heshima ya wanajeshi wa Ukraine na raia waliyouwawa katika vita vilivyoanzishwa kwa uchokozi wa Urusi," alisema Rais Poroshenko akihutubia mjini Kiev.

Sherehe za hapo jana (Jumanne 23 Agosti) zilizojumuisha gwaride kubwa la kijeshi, zilijiri wakati kukiwa na wasiwasi juu ya Urusi kuzidisha jeshi lake katika eneo linalopakana na nchi hizo mbili.

Aidha Rais Poroshenko aliweka shada maua mahala palipotokea vita, huku akisema "tunainamisha vichwa vyetu hii leo kwa watu waliyojitolea kupigania amani na mustakbali wa baadaye wa Ukraine".

Ukraine imekuwa ikipambana na watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi tangu mapema mwaka 2014, wakati Ukraine ilipomuondoa rais wale aliyeungwa mkono pia na Urusi, Viktor Yanuokovich, kufuatia maandamano makubwa yaliyotaka mahusiano ya karibu zaidi na nchi za Magharibi.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: Reuters/G. Garanich

"Nikiangalia nyuma zaidi ya miaka miwili ya vita, inawezekana kusema kwamba adui bado hajaweza kuifikisha Ukraine kupiga goti," alisema Poroshenko katika hotuba yake.

Rais huyo wa Ukraine aliyeungana na familia yake katika sherehe hizo pia aliuombea mustakbal wa baadaye wa Ukraine akiwa katika kanisa la kiorthodox mjini Kiev hii ikiwa ni kulingana na tovuti yake.

Mgogoro wa Ukraine waifanya Urusi kuwa matatani na mataifa ya Magharibi

Mnamo Agosti tarehe 24 mwaka 1991 bunge la Ukraine lilipitisha tamko lake la kutaka Uhuru na kuifanya nchi hiyo kujitenga na umoja wa kisovieti, na mikakati ya hivi karibuni ya kuisogeza Ukraine katika nchi za Magharibi imesababisha migawanyiko nchini humo ambapo Ukraine na baadhi ya mataifa ya Magharibi wameilaumu Urusi kwa mgawanyiko huo.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: picture alliance/empics/M. Dunham

Kiev pia ilipoteza eneo lake muhimu la Crimea lilipodhibitiwa na wanajeshi wa Urusi kufuatia amri iliyotolewa na Rais Vladimir Putin. Hatua hiyo ya Putin imeyaweka mahusiano yake na nchi za Magharibi katika msukosuko na kuingia katika vita baridi vilivyotoa changamoto katika jitihada za kutafuta suluhu ya migogoro mengine kama vile Syria.

Zaidi ya watu 9,500 wameuwawa na zaidi ya milioni mbili wamelazimika kuyahama makaazi yao kufuatia mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Ukraine na wanamgambo wanaoungwa mkono na Urusi katika miji mikubwa miwili ya kiviwanda katika eneo la Mashariki yanayodhibitiwa na wanamgambo hao tangu Aprili mwaka 2014. Hii leo Ukraine imeripoti kifo cha mwanajeshi wake kitu ambacho kimezidi kuongeza wasiwasi katika mapigano hayo.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef