Ukraine yaishambulia Urusi kwa droni 121
24 Januari 2025Pamoja na nguvu kubwa ya mashambulizi hayo lakini wizara hiyo haijazungumza chochote kuhusu athari zake. Lakini wizara imesema droni sita zimeharibiwa kwenye mkoa wa Moscow na nyingine katika eneo la jiji haswa, na nyingine zililenga mikoa mingine, ikiwa ni pamoja na ile inayopakana Ukraine na Kursk, ambapo askari wa Ukraine wanadhibiti eneo la ardhi licha ya juhudi za Urusi kuwaondoa.
Aidha wizara hiyo ilisema droni nyingine 20 pia zililenga eneo la Ryazan, kusini mashariki ya Moscow, ambapo taswira za matukio ambazo hazikuweza kuthibitishwa mara moja zilichapishwa katika mitandao ya kijamii. Kunaonekana moto mkubwa katika jiji hilo kadhalika kituo cha mafuta na cha umeme kimeshambuliwa.
Droni za Urusi zimewaua watu watatu mjini Kyiv
Wakati huo huo, jeshi la anga la Ukraine limesema limefanikiwa kudibiti shambulizi la Urusi la droni 25 kati ya 58 zilizorushwa usiku wa kuamkia leo. Wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine imesema mashambulizi hayo yamewaua wanaume wawili na mwanamke katika mkoa wa kati wa Kyiv, na kwamba mtu mwingine amejeruhiwa.
Katika hatua nyingine afisa mwandamizi katika nyanja ya usalama ya Urusi, Sergei Shoigu kuwa kitisho cha makabiliano ya silaha ya nyuklia baina ya mataifa yenye silaha hizo kinaongezeka.
Sergei Shoigu ambae ni mkuu wa baraza la usalama la Urusi ameliambia shirika la habari TASSkwamba kuongezeka kwa migogoro na kuzidi kwa ushindani wa kisiasa za kikanda duniani, kunazusha hatari za mapigano makali kati ya mataifa makubwa, ikiwa ni pamoja na kuhusishwa kukua kwa hofu ya matumzi ya nguvu za nyuklia.
Soma zaidi:Papa atoa wito wa kunyamazishwa kwa silaha
Waziri huyo wa zamani wa ulinzi amesema NATO inaongezeka shughuli za kijeshi karibu na Urusi na Belarus, na kufanya mazoezi ya kukera na vile vile matukio ya namna ya kujihami huko.
Na Jeshi la Korea Kusini lilisema linashuku Korea Kaskazini inajiandaa kutuma zaidi askari kwenda Urusi kupambana na vikosi vya Ukraine, hata baada ya kupoteza askari wake wengi na kushuhidia wengine wakiamatwa. Hata hivyo taarifa hiyo ya jeshi haikuwa na ufafanuzi wa kina wa namna gani Korea Kaskazini inaweza kulifanikisha hilo ikiwa ni takribani miezi miine tangu taifa hilo liripitwe kuwapelea askari wake Ukraine.
Vyanzo: RTR/AFP