1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za NATO 2025: Trump, Ukraine, matumizi ya ulinzi

Anchal Vohra | Hawa Bihoga
1 Januari 2025

Wakati NATO ikiukaribisha mwaka mpya, inakabiliwa na changamoto lukuki. Jumuiya hiyo inahitaji kuamua namna ya kuimarisha ulinzi wake dhidi ya Urusi, kuisadia Ukraine na kushughulika na Trump asiyetabirika.

https://p.dw.com/p/4oiNv
Poland | Bundeswehr inalinda sehemu ya upande wa mashariki wa NATO
Hivi karibuni Ujerumani iliidhinisha matumizi ya Euro bilioni 20 kununua vifaa vipya vya ulinzi, ikiwemo ununuzi wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot (inayoonekana hapa kwenye picha ya faili iliyopigwa Poland)Picha: Sebastian Kahnert/dpa/picture alliance

Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, aliweka vipaumbele vya muungano huo kwa mwaka 2025 katika hotuba ya kutisha akionyesha jinsi vita vilivyo karibu sana na mlango wa muungano huo wa kijeshi.

"Kutoka Brussels, inachukua siku moja tu kuendesha gari kufika Ukraine," alisema katika hotuba ya Desemba katika taasisi ya Carnegie Europe. "Huko ndiko mabomu ya Urusi yanaposhuka. Ndiko droni za Iran zinakorushwa. Na si mbali sana, wanajeshi wa Korea Kaskazini wanapigana."

Soma pia: Miaka 25 ya Rais Putin: Kwanza rafiki, na sasa adui

Rutte alitoa hoja ya kuungwa mkono kwa matumizi ya juu ya serikali kwenye ulinzi na uwekezaji siyo tu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa Ulaya, bali pia kuisaidia Ukraine na kuzuia Urusi kupanuka zaidi.

Je, matumizi ya juu ya ulinzi yatafanikiwa kumshawishi Trump?

Kuongezeka kwa matumizi ya ulinzi na wanachama wa Ulaya wa NATO pia kunaweza kuusaidia muungano huo kuipatia jawabu changamoto ya kumshughulikia Rais Mteule wa Marekani asiyetabirika, Donald Trump.

NATO yajadili jinsi ya kuipatia Ukraine silaha zaidi

Ingawa marais wote wa karibuni wa Marekani wamekuwa wakihimiza mataifa ya Ulaya kutumia zaidi kwenye ulinzi wao, Trump ndiye pekee aliyewahi kutishia kuacha wanachama wa muungano ambao hawajatekeleza ahadi zao.

Kwa lengo la kumshawishi Trump, mataifa mengi ya Ulaya yalitimiza ahadi ya kutumia asilimia 2 ya pato lao la taifa kwenye ulinzi mwaka 2024. Sasa, Trump anapojiandaa kurejea ofisini kwa muhula wa pili, kuna maoni kwamba NATO inaweza kuongeza lengo hilo hadi asilimia 3 au hata 4.

Soma pia: US kuiongezea Ukraine misaada kabla ya Trump kuingia madarakani

"Tutahitaji muda zaidi kushauriana kati ya washirika juu ya kiwango kipya hasa kitakavyokuwa. Lakini ni zaidi ya asilimia 2," Rutte alithibitisha. "Niwazi kabisa, ikiwa utatumia zaidi tu bila kutumia vizuri, unahitaji kufikia angalau asilimia 4."

Wataalamu wanasema Trump huenda akashinikiza asilimia 4, na kwamba washirika wa Ulaya wanapaswa kutoa mikataba ambayo anaiona kuwa ya manufaa.

"Ulaya inapaswa kutoa mpango mzuri kwa Marekani," Gesine Weber, mtafiti wa Mfuko wa Marshall wa Ujerumani, aliiambia DW katika taarifa ya maandishi.

"Mfumo ambapo Marekani inaweza kuwa 'njia ya mwisho' au 'mtetezi wa mwisho,' huku Wazungu wakihakikisha ulinzi wa kawaida wa Ulaya, unaweza kufanikisha kigezo hiki."

Trump: Ushindi huu ni mageuzi makubwa ya kisiasa

Juhudi za Ulaya kuiimarisha NATO — na changamoto zake

Kuna makubaliano kati ya wanachama wa NATO wa Ulaya kwamba wanapaswa kufanya zaidi kwa ajili ya ulinzi wao kwa kuimarisha uzalishaji wa vifaa vya ulinzi na kuziba mapengo ya vifaa vya kijeshi.

Mwaka 2024, NATO iliendesha zoezi lake kubwa zaidi la utayarifu wa kijeshi tangu Vita Baridi. Mnamo Desemba, iliamua kurekebisha mkakati wake wa vita vya mseto wa mwaka 2015 kutokana na kuongezeka kwa matukio ya uharibifu yanayoshukiwa kufanywa kwa niaba ya Moscow katika miaka ya hivi karibuni.

Pia, kumekuwa na juhudi za kuongeza idadi ya wanajeshi kwenye mipaka ya NATO. Ujerumani, kwa mfano, imeamua kutuma wanajeshi 5,000 nchini Lithuania ifikapo mwaka 2027.

Wanachama wa Ulaya wa NATO wanakabiliwa na changamoto kubwa hasa linapokuja suala la ujasusi, uchunguzi na uwezo wa ufuatiliaji, kama vile setilaiti zenye uwezo wa kuona maeneo ya adui au helikopta kubwa za usafirishaji zinazoweza kubeba vifaa vikubwa vya ulinzi na wanajeshi kwa umbali mrefu.

Maboresho yanapangwa kwa mwaka ujao katika sekta hii, lakini wataalamu wanaamini itachukua zaidi ya muongo mmoja kuendeleza uwezo ambao sasa Waulaya wanategemea kutoka kwa Marekani.

NATO ni nini?

"Ulaya ina setilaiti chache, na inaweza kuchukua hadi kati ya miaka 10 hadi 15 kuziba pengo hili," Rafael Loss, mtaalamu wa usalama na ulinzi katika eneo la Euro-Atlantic katika Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Ulaya, aliiambia DW.

Lakini changamoto ya kwanza kwa mataifa ya Ulaya ni kutoa fedha zinazohitajika kwa miradi hiyo, aliongeza.

Faida za NATO zinakwenda zaidi ya Atlantiki ya Kaskazini

Wanachama wa NATO wa Ulaya wanahoji kuwa muungano huo siyo tu unahakikisha usalama na ustawi pande zote za Atlantiki, bali pia unaimarisha mwitikio wa Washington kwa Beijing katika eneo la Indo-Pacific.

Washirika wameimarisha mahusiano na washirika wao wanne wa Asia — wanaojulikana kama AP4 ambao ni Australia, New Zealand, Korea Kusini na Japan — ili kupambana na ushirikiano wa "bila mipaka" wa China na Urusi. Ushirikiano wa NATO-AP4 unatarajiwa kukua mwaka 2025 kwa kushirikiana zaidi kwenye ujasusi.

Lithuania I Viongozi wa NATO
Viongozi wa Ushirikiano wa Asia na Pasifiki, pia unaojulikana kama AP4 ambao ni kundi la nchi nne muhimu washirika wa Asia-Pasifiki wa NATO -- Korea Kusini, Japan, Australia na New Zealand, wakiwa katika picha na aliekuwa Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg mjini Vilnius, Lithuania, Julai 12, 2023.Picha: Yonhap/picture alliance

"Wanachama wa NATO wa Ulaya wanajaribu kuwaambia wale wanaoipinga China ndani ya utawala wa Trump kwamba kuachana na NATO kutafanya iwe vigumu zaidi kwao kupambana na China," Loss alisema.

Trump atashughulikiaje suala la Ukraine?

Kadri uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unavyokaribia kumbukumbu ya mwaka wa tatu mwezi Februari, viongozi wa Ulaya wameelezea tena msaada wao kwa Kyiv lakini hawana matumaini kwamba endapo Marekani itakata msaada, wataweza kufidia pengo hilo.

Changamoto za bajeti nyumbani zimefanya mataifa tajiri ya Ulaya kuwa na hofu ya kutoa ahadi kwa Ukraine, hasa bila kujua kama msaada kutoka Marekani, mfadhili mkubwa wa kifedha na kijeshi wa Ukraine, utaendelea.

Uanachama wa Ukraine katika NATO pia utakuwa "dira kuu ya mvutano ndani ya muungano," Kristine Berzina, mkurugenzi mkuu wa GMF Geostrategy North aliyeko Washington, aliambia DW.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Wanachama wa Ulaya wa NATO kwa ujumla wanaunga mkono uanachama wa Ukraine katika muungano huo — huku Ujerumani ikiwa nje ya wigo huo — lakini dhamira hiyo itakuwa maneno matupu ikiwa utawala wa Trump utapinga upanuzi huo, Weber alisema.

Kwa mujibu wa Berzina, "(Rais wa Ukraine Volodymyr) Zelenskiy anaweka wazi kuwa mustakabali wa Ukraine unahitaji kuwa ndani ya NATO." Lakini akaongeza kuwa makamu wa rais ajaye wa Marekani, JD Vance, "ameonyesha mashaka kuhusu mwelekeo huu."

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwakaribisha Trump na Zelenskyy katika ufunguzi wa Kanisa Kuu la Notre Dame mwezi Desemba. Wataalamu walisema lengo lilikuwa kujaribu kubadili msimamo wa Trump juu ya Ukraine na kushawishi sera yake kwa manufaa ya Kyiv.

Lakini hakuna anayejua Trump atasonga vipi mbele — "hilo ndilo swali lisilo na majibu," alisema Loss.