1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaadhimisha miaka 31 ya Uhuru

24 Agosti 2022

Ukraine inaadhimisha miaka 31 tangu ijitangazie uhuru kutoka uliokuwa Muungano wa Sovieti, huku ikitimiza miezi sita kamili tangu kuvamiwa na kukaliwa kijeshi na jirani na mshirika wake wa zamani, Urusi.

https://p.dw.com/p/4FxhI
Ukraine-Krieg | Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ukraine Presidential Press Service/AFP

Kwenye hotuba iliyobeba hisia kali na kurushwa usiku wa kuamkia Jumatano (24 Agosti), Zelensky aliahidi kwamba Ukraine ingelipambana hadi tone la mwisho la damu wa raia wake, kwani haoni tena "mwisho wowote wa vita hivyo hadi pale nchi yake itakaposhinda."

Rais huyo alikiita kipindi cha miezi sita iliyopita tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza kuwa kipindi cha mabadiliko makubwa ndani na nje yaUkraine yaliyolisaidia taifa lake kujitambuwa na kuwatambuwa wengine.

"Katika miezi sita hii, tumeibadili historia, tumeubadili ulimwengu, na tumebadilika wenyewe. Sasa tunajuwa kwa yakini ni nani ndugu na rafiki yetu wa kweli, na nani siye hata jamaa wa dharura. Nani ambaye hakupoteza jina na heshima yake na nani aliwaogopea magaidi ili kujinusuru mwenyewe. Nani asiyetuhitaji na wapi mlango uko wazi kwa ajili yetu. Tumeelewa nani ni nani." Alisema.

Rais Zelensky alisema uvamizi wa Urusi dhidi yao ulioanza tarehe 24 Februari 2022 umeifanya Ukraine kuwa taifa lililozaliwa upya, na kwamba sasa kamwe lisingeacha tena kupigania uhuru wake dhidi ya utawala wa Moscow.

Akiwa amevalia fulana na suruwali yake ya kijeshi, rais huyo aliapa kwamba nchi yake ingelirejesha tena mamlaka yake kwa Rasi yaCrimea na mkowa mzima wa Donbas kwa njia yoyote itakayokuwa na kwamba hilo lisingehitaji ushauri ama ruhusa ya nchi nyengine yoyote.

"Donbas ni Ukraine. Na tutairejesha kwa njia yoyote iwayo. Crimea ni Ukraine. Na tutairejesha kwa njia yoyote iwayo. Ikiwa hutaki wanajeshi wenu wafe, basi ziwacheni ardhi zetu. Hamutaki mama zenu walie, basi ziwacheni ardhi zetu. Haya ndiyo masharti ya wazi na mepesi." Alisisitiza.

NATO yatuma salama za uhuru

Stoltenberg empfängt Serbiens Präsident Vucic
Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, Jens Stoltenberg.Picha: Olivier Matthys/AP/dpa/picture alliance

Hata hivyo, hotuba ya Zelensky ilikuja wakati mamlaka katika miji mikubwa muhimu ya nchi hiyo, Kyiv, Kharkiv na Mykolaiv zikipiga marufuku mikusanyiko yoyote ya kusherehekea Siku ya Uhuru hivi kwa kukhofia mashambulizi ya Urusi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, Jens Stoltenberg, alilipongeza jeshi la Ukraine kwa kile alichosema ni kujitowa kwao kupambana kwa ajili ya uhuru wa taifa.

Kupitia ujumbe kwa njia ya video uliosambazwa usiku wa kuamkia Jumatano, mkuu huyo wa muungano wa kijeshi unaoiunga mkono Ukraine kwenye vita vyake dhidi ya Urusi, alisema anatuma salamu za kheri kwa wote wanaopigania nchi yao.

"NATO itaendelea kuwasaidieni kadiri inavyohitajika, kwani Urusi haiwezi kuachwa ikashinda vita hivi.  Ukraine lazima ishinde na itashinda." Alisema.

Kwa upande mwengine, Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, amesema kasi ndogo ya kampeni yao ya kijeshi nchini Ukraine ni ya makusudi na inatokana na haja yao ya kupunguza idadi ya vifo vya raia.