1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine lazima iamue mustakabali wake yenyewe: Duda

22 Mei 2022

Rais wa Poland alisafiri kwenda Kyiv kuyaunga mkono malengo ya nchi za Magharibi na kuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kulihutubia bunge la Ukraine tangu kuanza vita hivyo.

https://p.dw.com/p/4Bhfc
Kiew Rede Polen Präsident Duda im Parlament der Ukraine
Picha: REUTERS

Wabunge wa Ukraine walimpigia makofu Rais wa Poland Andrzej Duda, ambaye aliwashukuru kwa heshima ya kuzungumza katika mahali ambapo "moyo wa Ukraine iliyo huru na ya kidemokrasia unapigia.”

Soma pia: Ukraine: Rais Volodymyr Zelensky asema diplomasia ndio njia pekee ya kuvimaliza vita

Ziara ya Duda, yake ya pili katika mji mkuu wa Ukraine tangu Aprili, imekuja wakati wanajeshi wa Urusi na Ukraine wakikabiliana kwenye eneo la mashariki la Donbas ambalo ndio kitovu cha viwanda la nchi hiyo.

"Licha ya uharibifu mkubwa, licha ya uhalifu wa kutisha na mateso makubwa ambayo watu wa Ukraine wanapitia kila siku, wavamizi wa Urusi hawajawavunja. Wameshindwa kuwaangusha. Na naamini kabisa kuwa hawatofaulu,” Duda aliliambia bunge la Ukraine la Verkhovna Rada. "Nataka kusema kwa nguvu zangu zote: ulimwengu huru una uso wa Ukraine hii leo.”

Ukraine-Krieg - Lyssytschansk
Makombora ya Urusi yamepiga eneo la LuhanskPicha: Leo Correa/dpa/AP/picture alliance

Poland imewakaribisha mamilioni ya wakimbizi wa Ukraine na kutumika kama lango la nchi za Magharibi kuingizia msaada wa kiutu na silaha kwenda Ukraine. Pia inatumika kama kituo cha kuingia Ukraine kwa baadhi ya wapiganaji wa kigeni, ikiwemo w akutoka Belarus, ambao wamejitolea kupigana dhidi ya wanajeshi wa Urusi.

Wakati huo huo, Ukraine imeirefusha hali ya dharura ya sheria ya kijeshi kwa miezi mitatu zaidi hadi Agosti 23 huku vita vyake na Urusi vikiendelea. Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky alitia saini kwa mara ya kwanza amri hiyo mnamo Februari 24 wakati walipovamiwa na vikosi vya Urusi.

Bunge la Ukraine limepiga kura kwa wingi kupitisha muswada huo unaoongezwa kwa mara ya tatu katika kipindi ambacho Urusi ikiendeleza mashambulizi yake na kulilenga eneo la mashariki la Donbas. Baada ya kushindwa kuudhibiti mji mkuu wa Kyiv, Moscow ilielekeza tangu mwezi Machi harakati zake mashariki mwa Ukraine.

Baada ya kutangaza udhibiti kamili wa kiwanda kikubwa cha chuma cha Azovstalkatika mji wa Mariupol ambacho kilikuwa ngome ya mwisho kwa wanajeshi waliokuwa wakiulinda mji huo wa bandari, jeshi la Urusi limeyapiga kwa makombora eneo hilo la kiviwanda kwa mfululuzo. Moscow inataka kulitanua eneo hilo ambalo limeshikiliwa tangu 2014 na wanaharakati wanaopigania kujitenga wakiungwa mkono na Urusi.

Ukraine Kiew | Selenskyj trifft irischen Parlamentschef
Zelensky amesema mapambano yanaendeleaPicha: Ukraine Presidency/Ukraine Presi/Planet Pix/Zuma/dpa/picture alliance

Katika ujumbe wake wa video kwa taifa Jumamosi usiku, Rais Volodymyr Zelensky ameelezea hali mjini Donbas kuwa "mbaya Zaidi,” lakini akasema uwezo wa nchi yake kuhimili karibu miezi mitatu ya vita kamili dhidi ya Urusi ni "Habari nzuri.”

Uwezekano wa Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya unatarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa kilele mjini Brussels mwezi Juni. Serikali mjini Warsaw inaongeza juhudi za kuwashawishi wanachama wengine wa EU ambao wanasitasita, kukubali nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita kuwa mwanachama.

Soma pia: Zelensky apendekeza makubaliano ya fidia kutoka Urusi

Mapema leo, Waziri wa Ufaransa anayehusika na maswala ya Ulaya Clément Baune, amesema leo kuwa jitihada ya Ukraine ya kujiunga na Umoja wa Ulaya haitakamilika kabla ya miaka 15 hadi 20 na hivyo kukataa matumaini ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ya kujiunga haraka EU kufuatia uvamizi wa Urusi katika nchi yake.

Reuters