1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine kusikiliza kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita

Josephat Charo
12 Mei 2022

Ukraine inajiandaa kusikiliza kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita dhidi ya mwanajeshi wa Urusi aliyekamatwa.

https://p.dw.com/p/4BA4o
Ukraine - ausgebrannter russischer Panzer in Kharkiv
Picha: Vitalii Hnidyi/REUTERS

Mwendesha mashitaka mkuu wa Ukraine Iryna Venediktova amesema afisi yake imemfungulia mashitaka sajini Vadin Shyshimarin, mwenye umri wa miaka 21, kuhusiana na mauaji ya raia wa umri wa miaka 62 ambaye hakuwa amejihami na silaha, aliyepigwa risasi alipokuwa akiendesha baiskeli yake mwezi Februari, siku nne baada ya uvamizi kuanza.

Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky ameukosoa vikali mpango wa eneo linalokaliwa na Urusi la Kherson kumtaka rais wa Urusi Vladimir Putin alijumuishe liwe sehemu ya Urusi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza katika hotuba yake ya jana jioni Zelensky alilaani watu ambao Urusi imewapata kuwa kama vibaraka na wanatoa kauli za kijinga kabisa. Zelensky aliongeza kuwa bila kujali watakachokifanya Warusi, hawana fursa yoyote na wana uhakika wa kuiokomboa nchi yao na watu wao.

Kherson ni eneo la kwanza kutwaliwa na Urusi tangu ilipoanza uvamizi wake Ukraine Februari mwaka huu, ikisema inataka kuipokonya silaha Ukraine na kuwalinda wazungumzaji lugha ya Kirusi kutokana na mafashisti. Hoja hiyo imepuuziliwa mbali na Ukraine na mataifa ya magharibi kama sababu isiyo na msingi kwa vita vya kikoloni vya kichokozi.

Utawala wa Kremlin umesema ni wajibu wa wakazi wanaoishi katika eneo hilo kuamua kama wanataka kujiunga na Urusi. Lakini Hennady Lahuta, gavana wa Kherson aliyetimuliwa amewaambia waandishi habari katika mji wa Dnipro nchini Ukraine kwamba wakaazi wanataka ukombozi wa haraka na warejee chini ya mbawa za nchi yao Ukraine.

Ukraine yapendekeza kubadilishana wafungwa na Urusi

Wakati haya yakiarifiwa Ukraine imependekeza mabadilishano na Urusi ili kuwakomboa wanajeshi wake ambao wamekuwa wakikilinda kiwanda kikubwa kabisa cha chuma cha pua cha Azovstal mjini Mariupol.

Ukraine-Krieg Mariupol | Stahlwerk Asovstal
Picha: AP/dpa/picture alliance

Naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk amesema kama hatua ya kwanza wameipa Urusi fursa hiyo na wangewasafirisha wanajeshi wao kupitia njia ya kibinadamu kutoka Azovstal. Pia amesema jeshi la Ukraine litawaachia huru wafungwa wa kivita wa Urusi kulingana na sheria zilizopo za mabadilishano. Kwa mujibu wa Vereshchuk mashauriano bado yanaendelea na hakuna makubaliano yaliyoafikiwa mpaka saa.

Wakati huo huo, Urusi imeyahimiza mashirika ya misaada kuwaondoa watu katika miji ya mashariki mwa Ukraine. Kanali Jenerali Mikhail Mizintsev wa wizara ya ulinzi ya Urusi amenukuliwa na shirika la habari la Urusi Interfax akisema jana jioni " kutokana na hali mbaya ya kibinadamu inayowakabili raia wengi katika miji ya Kramatorsk na Sloviansk, tunaitolea wito jumuiya ya kimataifa, Umoja wa Mataifa, shirika la ushirikiano wa usalama Ulaya OSCE na kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu kuchukua mara moja hatua zote kuwaondoa haraka na kwa usalama raia kutoka miji hii inayodhibitiwa na majeshi ya Ukraine".

Mizintsev amedai vikosi vya Ukraine vipo Kramatorsk na Sloviansk na wanatumia raia kama ngao ya kibinadamu. Amedai pia kuwa raia wapatao 90,000 bado wamo katika miji hiyo, ambayo inachukuliwa kuwa ngome za ulinzi wa Ukraine mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa upande mwingine kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amezungumza na rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky kuhusu jinsi serikali ya mjini Berlin inavyoweza kutoa msaada zaidi katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi. Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amesema katika taarifa kwamba viongozi hao wawili wamebadilishana mawazo kuhusu njia za kupeleka msaada zaidi Ukraine na kukubaliana kuendelea kuwa na mawasiliano ya karibu.

afp, ap, reuters