1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Je! uhalifu wa kivita unaweza kufafanuliwa kivipi?

Zainab Aziz Mhariri:n Saumu Yusuf
5 Aprili 2022

Uhalifu wa kivita ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu katika mzozo na matumizi ya silaha. Kwa maelezo yote, raia wanalengwa nchini Ukraine na hivi karibuni katika mitaa ya mjini Bucha.

https://p.dw.com/p/49Tfc
Ukraine | Leichen auf der Straße in Bucha
Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Maria Varaki mkurugenzi mwenza wa kikundi cha utafiti wa uhalifu wa kivita katika chuo cha King's College cha mjini London amefahamisha kuwa ufafanuzi wa uhalifu wa kivita dhidi ya raia umewekwa katika Kifungu cha 8 cha Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na unatokana na Mikataba ya Geneva ya 1949 na kwamba mikataba ya The Hague ya mwaka 1899 na 1907, chini ya kifungu cha mikataba ya kimataifa, imeweka sheria na kanuni ambazo zinapasa kuzingatiwa na pande zinazopigana.

Muonekano kwa nje wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague.
Muonekano kwa nje wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague.Picha: Vincent Isore/IP3press/imago images

Uhalifu wa Kivita

Varaki amesema wakati ambapo wanasiasa na waangalizi wanazungumzia juu ya uhalifu wa kivita unaofanywa nchini Ukraine ni lazima kwanza ushahidi uangaliwe mara mbili au zaidi hadi hilo kuthibitishwa kuwa ni uhalifu wa kivita lakini kwa sasa kinachowezekana ni kuzungumzia tu kuhusu madai ya uhalifu wa kivita.

Amesema wanasheria wanautaja uhalifu wa kivita kama ukiukaji mkubwa wa Mikataba ya Geneva. Kinachozungumzwa ni mauaji ya kukusudia ya raia, mateso, kuhusu watu kulazimika kuyahama makazi yao, na hata mashambulizi ya kiholela. Kwa sababu moja ya kanuni za msingi latika sheria ya vita ni kwamba raia hawapaswi kulengwa. Kwa maana hiyo, mashambulizi dhidi ya shule na wadi za wazazi huko mjini Kyiv au ukumbi wa michezo huko Mariupol yanafuzu kama ni ukiukaji wa sheria hizo.

Varaki ameeleza kuwa katika saa 48 zilizopita, wameshuhudiwa watu wakiwa wamevaa mavazi ya kiraia katika mitaa ya mji wa Bucha na baadhi yao wameuawa kwa kupigwa risasi nyuma ya vichwa vyao na haya yanadhihirisha kuwa ni ukatili chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Maeneo ya Kisheria ya Kijivu

Kuhusu maeneo ya kisheria ya kijivu, kwa maana ya eneo au hali ambayo ni vigumu kuhukumu kipi ni sahihi na kipi si sahihi. Varaki anaeleza kwamba, kama ilivyo kwa mambo mengi ya vita, kuna maeneo ya kijivu ndani ya ufafanuzi wa kile kinachofanya tukio kuwa ni uhalifu wa vita. Kwa ajili hiyo, sheria ya kimataifa ya kibinadamu inaongozwa na kanuni tatu - tofauti, uwiano na tahadhari - ambazo zinabainisha kuwa pande zinazohusika haziwezi kuwalenga raia au miundombinu ya kiraia. Ingawa kuna sheria za kuwapunguzia mateso wanadamu, kanuni hizo mara nyingi hutumiwa vibaya na hubadilishwa kirahisi.

Ubakaji na Unyanyasaji wa Kijinsia

Ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia unachukuliwa kuwa ni uhalifu wa kivita na uvunjaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu kwa mujibu wa Kifungu cha 27 cha Mkataba wa Geneva wa mwaka 1949. Mahakama za dharura na Mkataba wa Roma wa ICC unafafanua orodha ya kina juu ya uhalifu unaohusiana na jinsia. Azimio la Umoja wa Mataifa namba 1820 la mwaka 2008 linathibitisha tena kwamba ubakaji unaweza kuwa ni uhalifu wa kivita na silaha ya vita.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai wamesema watafungua uchunguzi kuhusu unyanyasaji wa kingono ulioripotiwa nchini Ukraine.Varaki amesema hapo kuna walakini, kutokana na kwamba ni jinsi gani swala hilo lingeweza kuratibiwa kwa urahisi kwa sababu wanaozungumziwa ni waathiriwa walio hatarini sana. Amesema kwa uelewa wake, Warusi walijaribu kuficha baadhi ya uhalifu huo kwa kuwachoma moto waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyeweka mkono kifuani akiwa na wanajeshi wake katika eneo la Bucha.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyeweka mkono kifuani akiwa na wanajeshi wake katika eneo la Bucha.Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Mhadhiri huyo wa maswala ya sheria ya kimataifa anasema japo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amevishutumu vikosi vya Urusi kwa kutekeleza mauaji ya halaiki lakini kisheria, ni vigumu sana kuthibitisha uhalifu wa mauaji ya kimbari na kwamba wanasiasa hutumia neno mauaji ya kimbari kwa madhumuni mengine lakini kisheria, ni vigumu sana kuthibitisha uhalifu wa mauaji ya halaiki.

Chanzo:  LINK: https://www.dw.com/a-61357154